
Na Edward Winchislaus, DODOMA
Wanavikundi wa mradi wa "TUINUKE PAMOJA" Mkoani Dodoma wameishauri jamii kuendelea kuwaamini wasichana na wanawake na kuwashirikisha katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili kuleta usawa wa kijinsia katika kazi.
Ushauri huo umetolewa leo jijini Dodoma waliposhiriki kongamano la kanda ya kati (Singida,Tabora na Dodoma) kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ambapo kilele chake kitaifa itakuwa Machi 8,2025 jijini Arusha.

Magret Lushakuzi ni Msaidizi wa mradi huo wenye lengo la kuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake ameiomba jamii kuachana na dhana ya kuwachukulia wanawake kama kundi didimizi lisiloweza kufanya miradi ya maendeleo.
Bi.Lushakuzi amesema kuwa kwa sasa mwanamke wanao uwezo wa kushiriki shughuli zote za kijamii na kiuchumi kisha kuleta maendeleo katika jamii na Taifa kwa ujumla.
"Mradi wetu wa TUINUKE PAMOJA una lengo la kuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika jamii,mradi huu katika mkoa wa Dodoma tumeanza na Wilaya ya Chemba, Kondoa mjini na Wilayani,Tamasha hili limetulenga kutokana na majukumu ya mradi wetu.
"Kundi la wanawake linapaswa kupewa kipaumbele kwa sababu kama mnavyojua kuwa mama ndiye msaada mkubwa kuanzia ngazi ya familia hadi kitaifa na hii tunaona kwa Tanzania tumepiga hatua mbalimbali Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan ni Mwanamke,kwa hiyo tulihitaji zaidi wanawake wapewe kipaumbele katika jamii zetu na wasichukuliwe kama watu dhaifu ambao hawawezi kutoa mchango wowote katika jamii na Taifa hivyo ni vyema wakapewa kipaumbele na kuwezeshwa",amesema Bi.Lushakuzi.
Pia ameongeza kuwa Jamii ilitumie kongamano hilo kutambua mchango wa wasichana na wanawake katika jamii na kuwapa kipaumbele katika Sekta zote huku akieleza kuwa katika nyanja ya uchumi wanawake wamekuwa hawapewi kipaumbele kama lilivyokundi la Vijana na wanaume.
Aidha amesema kuwa mara baada ya kongamano hilo mradi wa TUINUKE PAMOJA utazidi kuwafikia na kuwanufaisha wanawake wengi katika jamii kama ambavyo wamekwisha wafikia baadhi ya wanawake ambao tayari washajiunga katika vikundi mbalimbali chini ya Mradi huo.
Kwa upande wao wanavikundi wa mradi huo kutoka katika vikundi vitatu mkoani Dodoma ( Wilaya ya Chemba,Wilaya ya Kondoa na Kondoa mjini) wanaeleza kwa nyakati tofauti namna wanavyonufaika na mradi huo kimaendeleo huku wakiiomba jamii kutolibeza kundi la wanawake.
Habiba Masawe mwanakikundi cha Upendo kutoka Kondoa mjini ameeleza kuwa ushiriki wake leo umetokana nayeye kuwa mwanakikundi cha mradi wa TUINUKE PAMOJA huku akisema kuwa kupitia kongamano hilo amejifunza kuwa wanawake wakiwezeshwa wanaweza kutokana na wanawake wengi kushika nyadhifa za uongozi mbalimbali katika jamii.

Naye Shamira Athuman kutoka kikundi cha wanawake ( Kondoa Women Group) amesema kuwa Elimu aliyoipata kupitia kongamano hilo atahakikisha anawaelimisha wanawake wengine ambao hawakupata nafasi ya kushiriki kongamano la kuelekea kilele cha siki ya wanawake Duniani.
" Ushiriki wetu utakuwa chachu ya kuleta hamasa kwa wanawake wenzetu na mwisho kuzaa matunda mema,mimi Elimu yote niliyoipata hapa nitahakikisha nawafikishia wanawake wanakikundi wenzangu na wanakondoa wote",ameeleza Bi.Athuman.

Kwa upande wake Nasoro Abdallah kutoka kikundi cha The brothers Wilayani Kondoa amesema kupitia kongamano hilo wamejifunza namna nzuri ya kuandaa makongamano yenye lengo la kuwahamasisha wanawake huku akisema kuwa nao TUINUKE PAMOJA watahakikisha wanaandaa makongamano mbalimbali yenye lengo la kuwahamasisha wanawake dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
"Naishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe.Dkt.Samia kuendelea kuwapambania wanawake dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na mimi nitahakikisha nashirikiana vyema na wanakikundi wenzangu kuwapambania wanawake kufatia mafunzo ninayojifunza hapa pamoja na kuleta usawa wa kijinsia katika jamii",amesema Bwa.Abdallah.
Kongamano hilo limeenda sambamba na kaulimbiu isemayo wanawake na wasichana 2025,tuimarishe haki ,usawa na uwezeshaji ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mhe.Spika wa Bunge mstaafu Anne Makinda.


No comments:
Post a Comment