Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa( Mb.) amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TABD) na kufanya mazungumzo na yanayolenga kuendeleza ushirikiano kati ya wizara na benki hiyo na kuitaka kuendeleza miradi ya sekta za mifugo na uvuvi.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo 27 Januari 2026 katika ofisi ndogo ya Wizara hiyo iliyopo Kambarage Tower Jijini Dodoma, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TADB alifika kujitambulisha kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara hiyo na Benki ya TADB katika kuendeleza sekta za Mifugo na Uvuvi.
Katika Mazungumzo hayo Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameipongeza Benki ya TADB kwa jinsi inavyoshirikiana na wizara na kuiagiza kupanua wigo wa kuwasaidia wafugaji wadogo kupata mikopo nafuu ili waweze kuendeleza miradi yao, pamoja na kuongeza ushiriki wa Taasisi za kifedha kupitia TADB katika kutoa mikopo kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Bw. Frank Nyabundege amempongeza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kwa kuteuliwa kuwa Mbunge na Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kuahidi kuongeza kasi ya utoaji mikopo kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi hasa kwenye miradi inayowalenga vijana na wanawake.
Aidha, Bw. Nyabundege aliwasilisha taarifa fupi kuhusu ushiriki wa TADB katika Maendeleo ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi nchini ambapo kupitia TADB kama Benki ya Kisera inashirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuleta maendeleo katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi ikiwemo Benki kutoa mikopo ya mradi wa boti, ufugaji samaki kwa njia ya vizimba na mikopo ya vijana kupitia Programu ya BBT mifugo.
Kupitia mikopo ya miradi ya boti na vizimba TADB ilipokea kiasi cha Shilingi Bilioni 34.9 kwa ajili ya kutekeleza mradi ambapo hadi sasa kiasi cha Shilingi Bilioni 29.83 kimetolewa kwa wanufaika 5,932 katika mikoa 16 hapa nchini.
Aidha, TADB kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanikiwa kutoa jumla ya boti 219 na vizimba 536 kwa wanufaika wa miradi. Aidha, kwa kupitia mradi wa vijana wa BBT Mifugo, kiasi cha Shilingi Milioni 847.3 kimetolewa kwa wanufaika 106 kwa miradi ya mikopo isiyo na riba.
Bw. Nyabundege aliongezea kuwa TADB imewasilisha ushiriki wake katika kutoa mikopo katika Sekta ndogo ya Maziwa nchini kupitia Mradi wake wa TI3P ambapo kiasi cha Shilingi 40bn kimetolewa kwa wafugaji na wasindikaji wa maziwa nchini. Aidha, kupitia mradi wa TI3P TADB imefanikiwa kurekebisha na kujenga vituo 23 vya kukusanya maziwa vyenye thamani ya Shilingi 1.1bn kwa kushirikiana wafugaji,Wizara, Halmashauri na wasindikaji wa maziwa.






No comments:
Post a Comment