PSSSF YATUMIA SHILINGI BILIONI 75 KILA MWEZI KULIPA WASTAAFU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, March 21, 2025

PSSSF YATUMIA SHILINGI BILIONI 75 KILA MWEZI KULIPA WASTAAFU


Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unatumia kati ya shilingi bilioni 74 hadi 75 kila mwezi kwa malipo ya wastaafu.

Meneja Matekelezo wa PSSSF, Victor Kikoti, alibainisha hayo jijini Dodoma wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na PSSSF kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma (DPC) kuhusu maboresho ya huduma za mfuko huo.

Alisema katika daftari la wastaafu la mwezi uliopita, jumla ya wastaafu 100,076 walilipwa shilingi bilioni 75. Ameeleza kuwa kwa sasa malipo ya wastaafu hayana changamoto yoyote, na mfuko unalipa mafao kwa wakati.

“Mfuko sasa una miaka saba tangu kuanzishwa mwaka 2018. Tumetoka mahali ambapo tulikumbwa na changamoto nyingi, lakini kwa sasa tumeyashughulikia yote na mafao yanalipwa kwa wakati. Sheria inasema malipo yafanyike ndani ya siku 60 baada ya kustaafu, lakini sasa mfuko unalipa siku hiyo hiyo ya kustaafu,” alisema Kikoti.

Alifafanua kuwa maboresho yaliyofanywa katika mfumo wa uandikishaji wa wanachama yamewezesha malipo kufanyika kwa haraka zaidi.

Naye Meneja Mahusiano na Mawasiliano wa PSSSF, Isaya Mwakifulefule, alisema mafunzo hayo yalilenga kuwapa waandishi wa habari uelewa kuhusu maboresho makubwa katika utoaji wa huduma za mfuko huo.

“Tumewaeleza waandishi wa habari kuhusu changamoto zilizokuwepo wakati wa kuunganisha mifuko mwaka 2018. Katika kipindi cha mpito kulikuwa na changamoto za utendaji, lakini sasa zimetatuliwa na mfuko unakwenda vizuri,” alisema Mwakifulefule.


Awali, Mwenyekiti wa DPC, Mussa Yusuph, aliushukuru mfuko huo kwa mafunzo hayo na kusisitiza umuhimu wa elimu hiyo kutolewa mara kwa mara ili kuwasaidia wastaafu kupata taarifa sahihi kuhusu maboresho ya mfuko.







No comments:

Post a Comment