
Na Okuly Julius _DODOMA
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, serikali imewekeza shilingi bilioni 36.95 kuboresha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.
HUDUMA ZA TIBA ZA KIBINGWA NA TEKNOLOJIA YA KISASA
Akizungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka minne ndani ya Hospitali hiyo leo Machi 04, 2025 jijini Dodoma na waandishi wa habari, Prof. Makubi amesema Hospitali hiyo inatoa huduma za kibingwa na ubingwa wa juu kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Prof. Makubi amesema hospitali hiyo inajihusisha na mafunzo ya tiba pamoja na kufanya tafiti mbalimbali za uchunguzi na tiba za magonjwa ili kuboresha huduma za afya nchini.
MAFANIKIO KATIKA UPANDIKIZAJI FIGO
Pia, Pro. Makubi amesema Hospitali hiyo imeimarisha na kuboresha huduma ya upandikizaji wa figo, ambapo hadi sasa wagonjwa 25 kati ya 50 wamefanikiwa kupandikizwa figo kwa gharama ya shilingi milioni 875. Kati ya hao, wagonjwa 10 wamelipiwa matibabu hayo kupitia mfuko maalum wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa gharama ya shilingi milioni 350.
"iwapo wagonjwa hao wangepata huduma hiyo nje ya nchi, serikali ingelazimika kutumia shilingi bilioni 1.875. Hivyo, uwekezaji huo umeokoa shilingi bilioni 1," ameeleza Prof. Makubi
TAKWIMU ZA HUDUMA KWA WAGONJWA
Hospitali ya Benjamin Mkapa ina jumla ya watumishi 967, wakiwemo madaktari bingwa 81, madaktari bingwa wa juu 16, madaktari wa kawaida 65, na wauguzi 412. Hospitali hiyo ina vitanda 400 na kwa siku inahudumia wagonjwa wa nje 1,000–1,200, huku wagonjwa 250–300 wakilazwa.
Katika kipindi cha miaka minne, hospitali hiyo imehudumia wagonjwa 972,740, imetekeleza uchunguzi wa vipimo vya maabara 1,260,175, na vipimo vya radiolojia 272,660.
"Kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), hospitali yetu imepanua huduma za tiba za kibingwa na upasuaji kwa wananchi wapatao milioni 14 kutoka mikoa zaidi ya saba nchini," amesema Prof. Makubi
Pia, hospitali hiyo imerahisisha uvunaji wa figo kwa teknolojia ya kisasa ya matundu madogo (Laparoscopic Nephrectomy), huduma iliyoanza kutolewa Novemba 2024. Hatua hii imepunguza kwa 99% rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa huduma hizo.
UPANDIKIZAJI ULOTO KWA WAGONJWA WA SIKOSELII
Amesema mnamo Januari 4, 2024, hospitali hiyo ilianzisha huduma za upandikizaji uloto kwa wagonjwa wa sikoseli, ambapo watoto 20 wamenufaika na kupona ugonjwa huo. Mpango huo umetumia shilingi bilioni 1.1, huku kiasi hicho kikiwa chini ya shilingi bilioni 2.1 ambacho kingetumika endapo wagonjwa hao wangepata huduma hiyo nje ya nchi. Hivyo, serikali imeokoa shilingi bilioni 1.
"Katika kuadhimisha Wiki ya Wanawake Duniani, Prof. Makubi ametoa pongezi kwa wanawake waliowezesha huduma hiyo, akiwemo Mhe. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Stellah Malangahe, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Damu na Upandikizaji Uloto katika hospitali hiyo," amesema Prof. Makubi
MWELEKEO WA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA
Hospitali ya Benjamin Mkapa imejipanga kupandishwa hadhi kufikia kiwango cha Hospitali ya Taifa. Mpango wake ni kuimarisha mifumo ya TEHAMA ili kuboresha huduma, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia ya akili bandia (AI) katika huduma za wauguzi, huduma kwa wateja, upasuaji wa kisasa kwa roboti (robotic surgeries), na upasuaji wa matundu madogo.
Vilevile, hospitali hiyo inatekeleza miradi mikakati ya miundombinu, ikiwa ni pamoja na:
Ujenzi wa vituo vya umahiri vya upandikizaji figo (kwa ushirikiano na Japan),
Kituo cha upandikizaji uloto (EAC),
Upasuaji wa moyo, ubongo, ENT, afya ya mama na mtoto, na tiba ya macho,
Ujenzi wa hosteli kwa ajili ya wagonjwa na wageni.
USHIRIKIANO NA TAASISI ZA NDANI NA NJE YA NCHI
Hospitali ya Benjamin Mkapa pia ina mkakati wa kupanua diplomasia ya afya kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi. Hadi sasa, hospitali hiyo inashirikiana na taasisi za ndani kama UDOM, Muhimbili, KCMC, na Bugando, pamoja na wadau wa kimataifa kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalamu wa afya nchini.
Kituo cha upandikizaji uloto (EAC),
Upasuaji wa moyo, ubongo, ENT, afya ya mama na mtoto, na tiba ya macho,
Ujenzi wa hosteli kwa ajili ya wagonjwa na wageni.
USHIRIKIANO NA TAASISI ZA NDANI NA NJE YA NCHI
Hospitali ya Benjamin Mkapa pia ina mkakati wa kupanua diplomasia ya afya kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi. Hadi sasa, hospitali hiyo inashirikiana na taasisi za ndani kama UDOM, Muhimbili, KCMC, na Bugando, pamoja na wadau wa kimataifa kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalamu wa afya nchini.
No comments:
Post a Comment