
Na Okuly Julius - Dodoma
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amesema kuwa sekta ya madini imeendelea kukua kwa kasi katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, jambo lililosaidia kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa na mapato ya serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka minne ndani ya sekta Madini, Mhandisi Lwamo amesema kuwa makusanyo ya maduhuli ya serikali kutoka sekta ya madini yameongezeka kutoka shilingi bilioni 624.61 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 753.82 mwaka wa fedha 2023/2024.
"Ukuaji wa sekta ya madini umeendelea kuimarika, ambapo mchango wake katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 mwaka 2021 hadi asilimia 9 mwaka 2023, huku ukuaji wa sekta yenyewe ukiongezeka kutoka asilimia 9.4 mwaka 2021 hadi asilimia 11.3 mwaka 2023," amesema Mhandisi Lwamo.
Ameongeza kuwa kutokana na jitihada zinazoendelea kufanywa na serikali kupitia tume hiyo, mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa unatarajiwa kufikia asilimia 10 na zaidi ifikapo mwaka 2025.
Amesema takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022, mauzo ya madini katika masoko na vituo vya ununuzi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 2,361.80 hadi kufikia shilingi bilioni 2,597.18 kwa mwaka 2023/2024.
"Hili linaonyesha wazi kuwa juhudi za serikali za kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini zimeleta matokeo chanya, ikiwemo kudhibiti biashara holela ya madini na kuongeza uwazi katika masoko," alisema.
Mhandisi Lwamo amesema, katika kipindi cha miaka minne, sekta ya madini imezalisha ajira 19,874, ambapo kati ya hizo, 19,371 ni za Watanzania. Mhandisi Lwamo amesema kuwa tume imeendelea kusimamia kikamilifu ajira kwa Watanzania katika kampuni za uchimbaji wa madini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi.
Amesema Tume ya Madini pia imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wachimbaji wadogo, ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo mahsusi kwa ajili yao.
"Tume imefanikiwa kutenga maeneo 58 katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya wachimbaji wadogo, pamoja na kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili waweze kupata mikopo ya kuendeleza shughuli zao za uchimbaji," amesema Mhandisi Lwamo.
Aidha, tume imefanikiwa kutoa jumla ya leseni 41,424 katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, ikizidi lengo la leseni 37,318 zilizopangwa kutolewa, ikiwa ni sawa na asilimia 111. Leseni hizo zinajumuisha leseni za uchimbaji mkubwa, wa kati, na mdogo.
Mhandisi Lwamo amesisitiza kuwa sekta ya madini ni miongoni mwa sekta muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa na kuboresha maisha ya wananchi.
"Tunaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha sekta ya madini inazidi kuwa chachu ya maendeleo ya jamii na uchumi wa nchi kwa ujumla," amesema.
Tume ya Madini inaendelea kufanya kazi kwa karibu na wachimbaji, wawekezaji, na wadau wengine ili kuhakikisha sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya Taifa.



No comments:
Post a Comment