Na Mwandishi Wetu _ Dar es Salaam
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umepata mafanikio ya kuimarisha upitikaji wa miundombinu ya barabara za wilaya wenye urefu wa kilometa 144,429.77 kwa asilimia 55 ambapo lengo ni kufikia asilimia 60 ifikapo mwezi Juni, 2025.
Mafanikio haya yanatokana na ongezeko kubwa la bajeti ya Wakala kutoka shilingi bilioni 275 hadi shilingi bilioni 870.3 sawa na ongezeko la asilimia 216 kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2024/25.
Hayo yameelezwa leo tarehe 26/03/2025 Jijini Dar es Salaam na Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo ambaye pia ni Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga katika semina iliyoandaliwa na TARURA kwaajili ya Wahariri wa Vyombo vya Habari.
“Mtandao wa barabara za lami katika kipindi hicho umeongezeka kutoka Km. 2,025.69 hadi Km. 3,337.66, na changarawe kutoka Km. 27,809.26 hadi Km. 42,059.17 na barabara za udongo zimepungua kutoka Km. 112,317.20 hadi Km. 99,032.93. Madaraja yaliyojengwa yamefikia 3,195 na makalavati 75,620,” amesema Mhandisi Mkinga.
Aidha, amesema katika ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na Wakala wameendelea kufanya majaribio kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ya mawe 'cobble stone roads' na madaraja ya mawe 'stone arch bridges' pamoja na teknolojia nyingine katika kuboresha barabara wanazozisimamia.
Ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia na malighafi za ujenzi zinazopatikana eneo la kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya barabara, huongeza ufanisi, huokoa muda, hutunza mazingira kwa gharama nafuu.
“Matumizi ya teknolojia mbadala na malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi kwaajili ya ujenzi wa barabara na madaraja imeweza kupunguza gharama zaidi ya 50% ambapo TARURA imeweka kipaumbele cha kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupunguza gharama za ujenzi,” amesema
Hata hivyo Wakala umeendelea na matumizi ya malighafi za ujenzi wa barabara zinazopatikana maeneo ya kazi na utafiti wa teknolojia mbadala za ECOROADS, Ecozyme, na GeoPolymer kwenye ujenzi wa barabara kwa lengo la kupata ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kulinda mazingira, amesema Mhandisi Mkinga.
Amesema jumla ya madaraja ya mawe 350 yamejengwa ambapo gharama zimepungua kwa kiasi cha Shilingi bilioni 10. Kwa upande wa majaribio ya teknolojia mbadala Km. 7.95 zimekamilika na Km. 53.76 zipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na ufuatiliaji wa ubora wa teknolojia hizo unaendelea.
“Haya yote ni matokeo ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mtandao wa barabara za wilaya, kwa kuwa maeneo ya kilimo vijijini yakiwa yanafikika kwa mwaka mzima, inaongeza ukuaji wa kilimo na kupunguza umaskini,”
No comments:
Post a Comment