HELIUM ONE YAKAMILISHA MALIPO YA FIDIA KWA WANANCHI WA ITUMBULA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 24, 2025

HELIUM ONE YAKAMILISHA MALIPO YA FIDIA KWA WANANCHI WA ITUMBULA



● Yalipa fidia ya shilingi zaidi ya milioni 100 kwa wananchi

● Wananchi wafurahishwa na maendeleo ya mradi

● Mradi kutekelezwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10


Na Mwandishi Wetu Momba, Songwe


Kampuni ya Helium One, inayojihusisha na utafiti na uchimbaji wa gesi ya helium nchini Tanzania, imekamilisha zoezi la ulipaji fidia ya zaidi ya milioni 100 kwa wananchi wa Vijiji vya Itumbula, Lwatwe, Masanyinta, Mkonko na Muungano Wilaya ya Momba mkoani Songwe, waliopisha shughuli za maendeleo ya mradi huo.

Akizungumza leo Aprili 24, 2025 wakati wa ziara ya wataalam kutoka Wizara ya Madini pamoja na waandishi wa habari, Msimamizi katika maeneo ya utafiti na Uendelezaji wa Mradi huo, Emmanuel Ghachocha, alisema kuwa fidia hiyo imelipwa kwa mujibu wa sheria za nchi na imelenga kuwawezesha wananchi waliotoa maeneo yao kwa ajili ya shughuli za utafiti na uchimbaji.

Kwa mujibu wa Ghachocha, mradi huo ulianza rasmi mwaka 2015 kampuni ya Helium One ilipoanzishwa nakufanikiwa kufanya shughuli zake za kitafiti ikiwamo utafiti kwa njia ya mitetemo na uchimbaji wa visima vya utafiti. Kuanzia mwaka 2021 mpaka 2025 Kampuni ya Helium One imekwisha chimba visima vinne, ambapo mafanikio makubwa yalionekana kwenye visima vya Itumbula West 1 na Tai 3 vilivyogundulika kuwa na mkusanyiko mkubwa wa gesi ya helium.

Baada ya kufanyika majaribio (Extended Well Testing) Kisima cha Itambula 1 ilionesha kuwa na mkusanyiko wa gesi hiyo ya helium yenye kiwango cha asilimia 7.9%. Utafiti wa kina uliofuata pia ulionesha uwepo wa mkusanyiko wa gesi hiyo ya helium kwa kiwango cha asilimia 5.5 juu ya ardhi ikitokea kisimani.

“Mradi huu unatarajiwa kudumu kwa takribani kipindi cha zaidi ya miaka 10 ya uendelezaji na uzalishaji wa gesi hiyo,” alisema Ghachocha.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Songwe, Mjiolojia Chone Malembo, alisema kuwa Songwe ina nafasi kubwa ya kuwa kinara wa uzalishaji wa gesi ya helium nchini, jambo ambalo litaongeza mchango wa mkoa huo katika Pato la Taifa kupitia sekta ya madini.

Sambamba na hapo, Malembo alibainisha kuwa, katika mwaka 2023/2024, mkoa ulikusanya zaidi ya shilingi bilioni 37 kutokana na shughuli za madini na kwa robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 ukikusanya zaidi ya bilioni 36, na matarajio ni kufikia bilioni 40 ifikapo mwisho wa mwaka huu wa fedha.

Naye, Mjiolojia kutoka Wizara ya Madini, Venosa Ngowi, ameeleza kuwa, Tanzania imebarikiwa kuwa Gesi ya helium katika maeneo mbali mbali ikiwemo katika Bonde la Ziwa Rukwa na Bonde la Eyasi Wembere.

Ngowi amefafanua kuwa, gesi hiyo ina matumizi muhimu katika sekta mbalimbali ikiwemo afya (hasa kwenye MRI Scanner), teknolojia ya anga, utafiti wa sayansi ya angahewa, pamoja na usafiri wa anga kama vile roketi na vifaa vya ndege.

Aidha, Wananchi wa eneo husika wameishukuru Serikali na Kampuni ya Helium one kwa kukamilisha kulipa fidia kwa wananchi waliopisha meadi.

“Tulikuwa na wasiwasi mwanzoni kama tutalipwa stahiki zetu, lakini sasa tunashukuru. Tumepata fidia zetu na tunaona namna mradi huu utakavyosaidia maendeleo ya kijiji chetu.”

Mzee Suleiman Mwashiuya, mkazi wa kijiji hicho, amesema: “Huu ni mradi wa kihistoria kwa eneo letu. Mbali na fidia, tunatarajia vijana wetu kupata ajira, na huduma za kijamii kama barabara na maji kuimarika kutokana na uwepo wa mradi.”

Kwa sasa, nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa gesi ya helium duniani ni Marekani, Urusi, Qatar, Saudi Arabia na Algeria.




No comments:

Post a Comment