
Na Mwandishi Wetu , Dodoma
Katika kuendelea kuadhimisha Wiki ya Afya Kitaifa inayoendelea Jijini Dodoma kuanzia tarehe 3 hadi 8 Aprili, wananchi kwa wingi wamejitokeza leo kushiriki kwenye matembezi maalum ya kuhamasisha mazoezi ya viungo kama njia ya kujikinga dhidi ya magonjwa Yasiyoambukiza.
Matembezi haya yameanzia katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC) na kupitia njia mbalimbali ikiwemo Railway, Kilimani, IRDP (Furaha Campus), Safina Round About, Kimbinyiko, VETA, na kurejea tena JKCC.
Matembezi haya yameongozwa na Kaimu Mkurugenzi Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Otilia Gowelle pamoja na Washiriki wengine ambao ni watumishi wa sekta ya afya, wanafunzi, vikundi vya mazoezi, viongozi wa serikali, watumishi wa kada mbalimbali na wananchi kwa ujumla.
Lengo kuu la zoezi hili ni kuhimiza wananchi kuelewa umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara ili kujikinga dhidi ya magonjwa sugu yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, unene kupita kiasi na magonjwa ya moyo.
Wiki ya Afya Kitaifa 2025, inayobeba kaulimbiu “Tulipotoka, Tulipo, Tunapoeleka; Tunajenga Taifa Imara Lenye Afya”, inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma za afya, umuhimu wa lishe bora, chanjo, usafi wa mazingira, na mbinu za kuzuia magonjwa mbalimbali.
Matembezi haya ni sehemu ya matukio mbalimbali yaliyoandaliwa kuelekea kilele cha maadhimisho hayo yatakayofanyika tarehe 8 Aprili, 2025.















No comments:
Post a Comment