Na Mwandishi wetu-Morogoro
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendesha mafunzo ya siku tatu kwa Watumishi 100 waliopo katika Taasisi Rekebu zinazohusika na uboreshaji wa mazingira ya biashara na Uwekezaji nchini, ili kuwaongezea ujuzi na kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo hayo yamefunguliwa leo tarehe 28 Aprili, 2025 mjini Morogoro na mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maadili, Bi. Leila Mavika.
Bi. Mavika amesema mafunzo hayo yanafanyika kufuatia eneo hilo kuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kutumia muda mwingi na gharama kubwa za kifedha wakati wa kuanzisha na kuendesha biashara, uwepo wa taratibu nyingi na zinazojirudia zinazotakiwa kufuatwa na wawekezaji, pamoja na mapungufu katika baadhi ya Sheria na Kanuni zinazotumiwa na Taasisi Rekebu.
Amesema pamoja na mambo mengine, ilionekana masuala hayo yakifanyiwa kazi yatawezesha Nchi kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia biashara ambayo yatavutia wawekezaji wengi zaidi.
Bi. Leila ameongeza kuwa, Serikali imeanza utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Uwekezaji na Mazingira ya Biashara (MKUMBI) awamu ya Kwanza kwa lengo la kufanya mageuzi na kuboresha Mazingira ya Biashara nchini Tanzania ili kuwapunguzia mzigo na vihatarishi wafanyabiashara kwa kuhusianisha mifumo ya udhibiti wa biashara ili kuzuia uwepo wa taratibu nyingi zinazojirudia na mwingiliano wa majukumu ndani ya Taasisi Rekebu na kuhakikisha kunakuwepo na uwazi wa mifumo ya udhibiti wa uwekezaji na biashara kupitia majukwaa mbalimbali ya TEHAMA ambayo hutoa taarifa za taratibu za udhibiti kwa Umma.
Amesema Ofisini hiyo ni mojawapo ya Taasisi iliyopo katika Mpango huu kutokana na jukumu ililonalo la kusimamia mafunzo katika Utumishi wa Umma kwa mujibu wa Hati idhini ya uanzishwaji wa Wizara.
Amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024, Ofisi ya Rais-UTUMISHI ilifanya survey kwa baadhi ya Taasisi Rekebu 31 ili kukusanya taarifa za upungufu wa ujuzi katika Taasisi hizo na kuchukua hatua stahiki za kuondosha upungufu huo.
Mafunzo yanayoanza leo yamejikita katika kushughulikia maeneo ya upungufu wa ujuzi yaliobainishwa na survey hiyo ambayo ni Mafunzo mbalimbali kama vile Kuimarisha Mazingira ya Uwekezaji; Ujuzi wa Majadiliano (Negotiation Skills); Utunzaji na Matumizi Sahihi na Salama ya Nyaraka na Kumbukumbu; Uwezo wa Kufikiri Kimkakati na Utoaji wa Maamuzi Sahihi; Utunzaji wa Muda; Namna ya Kuwa Mtumishi wa Thamani katika Taasisi; Akili Hisia; Huduma kwa Mteja na mengine mengi.
Bi. Mavika amewataka Watumishi wote ambao wanahudumu katika Taasisi Rekebu kuzingatia Maadili ya Utumishi wa Umma wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kutumia lugha nzuri, bila upendeleo na kuepuka RUSHWA ili kulinda taswira na heshima ya Utumishi wa Umma na Taifa kwa ujumla.
“Ni Imani yangu kuwa uchaguzi wa Taasisi hizi haukuwa wa bahati mbaya bali ni wenye makusudi mahsusi yenye dhamira ya kuboresha utendaji kazi wenu kwa kuwaongezea ujuzi ili kuhakikisha Taasisi zenu zinatengeneza mazingira rafiki na wezeshi kwa Wawekezaji wanaokuja kupata huduma.” Amesisitiza Bi. Mavika.
Amesema uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji Biashara na Uwekezaji katika nchi yetu ni jambo la muhimu kwa kuwa ni eneo linalowezesha Serikali kupata mapato na kuboresha huduma kwa Wananchi.
Mwaka 2018, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ilizindua Mpango wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara, Mpango ambao uliwezesha nchi kufanya mapitio ya mfumo wa mazingira wezeshi ya biashara (BEE) kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara.
No comments:
Post a Comment