Na Okuly Julius _ DODOMA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeazimia kuongeza fursa za mafunzo ya amali kwa Watanzania kupitia vyuo vya ufundi stadi (VETA).
Akizungumza jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Shirika la Watetezi wa Mama, Prof. Mkenda alisema kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vipya 64 vya VETA ili kuhakikisha kila wilaya inakuwa na chuo cha kutoa mafunzo ya amali. Aidha, alieleza kuwa Serikali imeongeza wigo wa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya diploma ili kuwasaidia kupata ujuzi utakaowawezesha kushindana katika soko la ajira.
Prof. Mkenda alisema hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo inayolenga kuwajengea wanafunzi ujuzi na maarifa ya kuchangia maendeleo ya taifa.
“Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umechochea mageuzi makubwa katika elimu. Tumeshuhudia ujio wa Sera mpya ya Elimu inayolenga kuzalisha wahitimu mahiri na wenye ujuzi,” alisema Prof. Mkenda.
Aliongeza kuwa hatua nyingine madhubuti ni kuongeza muda wa elimu ya lazima hadi kufikia miaka 10, sambamba na kuimarisha mitaala ya elimu ili iendane na mahitaji ya sasa ya kiuchumi na kijamii.
Serikali pia inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu katika ngazi zote kama sehemu ya mkakati wa kuhakikisha elimu bora na jumuishi inapatikana kwa Watanzania wote.
No comments:
Post a Comment