
Na Okuly Julius _ DODOMA
Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde ,amesema mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa umeongezeka na kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024, ikiwa ni mafanikio makubwa yaliyotimia mwaka mmoja kabla ya lengo lililowekwa kufikiwa ifikapo mwaka 2025.
Mavunde ameyasema hayo leo Aprili 23,2025 jijini Dodoma , wakati akizungumza na waandishi wa habari,ambapo ameeleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Mheshimiwa Rais amedhihirisha nia ya kweli ya kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kusimamia rasilimali zetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Ameendelea kusisitiza uwajibikaji, utawala bora na mshikamano wa kitaifa – misingi ambayo imechochea ufanisi katika utendaji wetu wa kila siku,” alisema Waziri huyo.
Mavunde ameeleza baadhi ya hatua za kimkakati zilizochangia mafanikio hayo ni pamoja na: "Kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli kutoka kwenye shughuli za madini,Kuanzishwa kwa minada rasmi ya madini ya vito,Udhibiti wa utoroshwaji wa madini nje ya nchi.
Pamoja na hayo Waziri Mavunde amesema kuongezeka kwa vituo vya ununuzi na masoko ya madini kote nchini na kuanza kwa ununuzi wa dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania.
Waziri amewataka wawekezaji wote wanaofanya kazi katika sekta hiyo kuendelea kuzingatia matakwa ya Sheria ya Madini, Sura ya 123, akibainisha kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wote – wa ndani na wa kigeni – wenye nia njema ya kuwekeza kwa tija na kuchangia ustawi wa uchumi wa Taifa.
Waziri amesema: “Namba hazidanganyi. Mchango wa sekta hii katika Pato la Taifa sasa umefikia lengo tulilolikusudia miaka kadhaa iliyopita. Ni matumaini yetu kuwa kwa mwendo huu, Sekta ya Madini itaendelea kuwa mhimili mkuu wa uchumi na chanzo kikuu cha fedha za kigeni nchini.”




No comments:
Post a Comment