WAZIRI AWESO AAGIZA UTAFITI WA MAJI KATA YA MKONZE KUMALIZA MGAO DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 18, 2025

WAZIRI AWESO AAGIZA UTAFITI WA MAJI KATA YA MKONZE KUMALIZA MGAO DODOMA



Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amewataka watafiti wa maji kuhakikisha wanatafiti eneo lolote ndani ya Kata ya Mkonze ili kufanikisha wakazi wa eneo hilo wanapata huduma ya maji safi na salama.

Agizo hilo amelitoa Aprili 17, 2025, katika ziara yake ya kukabidhi mitambo ya kuchimbia visima eneo la Mkonze na kukagua miradi ya uchimbaji wa visima vya maji pembezoni mwa mji, ikiwa ni hatua ya muda mfupi ya kumaliza tatizo la mgao wa maji katika Jiji la Dodoma.

Akizungumza mbele ya wananchi wa kata hiyo, Mhe. Aweso amesema tayari wameshafanya mazungumzo na watafiti na wachimbaji wa visima vya maji na wamekubaliana kufanya kazi bila kisingizio chochote.

Ameeleza kuwa, licha ya eneo hilo kuwa na maji machache kiasili, wataalamu hao wanapaswa kuhakikisha wanafanikisha upatikanaji wa maji katika Kata ya Mkonze.


Mapema katika ziara hiyo, Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema hatua iliyopo sasa ni kuhakikisha uzalishaji wa maji lita milioni 28 unafikiwa ili kukidhi mahitaji ya sasa ya maji na kumaliza tatizo la mgao.

Aidha, amemshukuru Waziri wa Maji kwa hatua ya kufanya ziara ya siku tatu ndani ya jimbo hilo na kufuatilia hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ili kusaidia kuongeza uzalishaji mali kwa wananchi.

Baadhi ya wananchi wa kata hiyo, akiwemo Glad Siwani na Salome Ndaga, wamesema adha ya maji imekuwepo kwa muda mrefu, lakini ujio wa Waziri wa Maji ni ishara njema ya matumaini ya kupata huduma ya maji safi na salama kwa ukaribu.

Pamoja na hayo, wameomba mamlaka zilizopewa jukumu la uchimbaji wa visima hivyo kufanya kazi kwa haraka ili kusaidia kupunguza gharama na umbali wa upatikanaji wa maji.

Uchimbaji wa visima vya maji pembezoni mwa Jiji la Dodoma ni mojawapo ya mikakati ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Dodoma kumaliza tatizo la mgao wa maji katika maeneo mbalimbali.




No comments:

Post a Comment