
Na Mwandishi Wetu_ DODOMA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka minne katika maeneo mbalimbali.
Amesema mafanikio hayo yanatokana na azma ya Rais ya kuujenga Utumishi wa Umma wenye tija katika maendeleo ya taifa.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo Aprili 17, 2025, wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na usimamizi wa Mikataba ya Utendaji Kazi Serikalini kupitia mfumo wa e-UTENDAJI (PEPMIS/PIPMIS) unaolenga kubaini kiwango cha utendaji kazi na uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa umma.
Aidha, Serikali imefanikiwa kuanzisha Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu (HR-Assessment) ambao husaidia kubaini idadi sahihi ya watumishi katika kila kituo cha kazi ili kuwezesha utekelezaji bora wa majukumu.
Kuhusu maslahi na stahiki za watumishi wa umma, Mhe. Simbachawene amesema Rais Samia amefanya maboresho makubwa ikiwemo kupunguza PAYE kutoka asilimia 9 hadi 8, kufuta tozo ya 6% kwa waliopata mikopo ya elimu ya juu, kulipa malimbikizo ya mishahara, kupandisha vyeo, kubadilisha kada, na kuanzishwa kwa mfumo wa “Watumishi Portal” kwa ajili ya kutoa huduma za kiutumishi kidijitali.
Hadi kufikia Machi 31, 2025, madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 148,137 yenye jumla ya Sh. 248.5 bilioni yalishughulikiwa, pamoja na malimbikizo ya wastaafu 10,022 yenye thamani ya Sh. 33.2 bilioni.
Katika kipindi hicho, watumishi 610,733 walipandishwa vyeo, 42,515 walibadilishwa kada, 133,317 waliajiriwa, na vibali vya ajira mbadala 41,673 vilitolewa.

Kwa upande wa TASAF, jumla ya miradi 27,863 ya kutoa ajira za muda kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ilitekelezwa hadi Desemba 2024.
Mhe. Simbachawene pia ameipongeza TAKUKURU kwa utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi kupitia programu ya “TAKUKURU Rafiki” iliyoimarisha mapambano dhidi ya rushwa katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wa TEHAMA, Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imetekeleza agizo la Rais kwa kuanzisha Mfumo wa Pamoja wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (GovESB) ambao umeziwezesha taasisi 179 za umma na mifumo 202 kuwasiliana na kubadilishana taarifa, hususan taasisi za sekta ya haki jinai.
Mhe. Simbachawene amempongeza Rais Samia kwa uongozi wake madhubuti na kusimamia utekelezaji wa maelekezo yake kwa ufanisi mkubwa katika kuimarisha utumishi wa umma nchini.

No comments:
Post a Comment