Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Mwenyekiti wa Bonanza Mahala Pa Kazi, Denis Manumbu, ametoa wito kwa viongozi wa taasisi za serikali kote nchini kuhakikisha wanahamasisha na kuwaruhusu watumishi wao kushiriki kikamilifu katika mazoezi, hususan Bonanza la Mahala pa Kazi, akisema kuwa ushiriki huo unachangia kuongeza ufanisi kazini.
Bonanza hilo ambalo hufanyika kila mwisho wa mwezi jijini Dodoma, limewakutanisha watumishi kutoka taasisi na idara mbalimbali za serikali takriban 11.
Miongoni mwao ni pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, RAS Manyara, DED Bahi, Tume ya Uwapatanishi, Wizara ya Maji, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ujenzi, Mahakama na taasisi nyinginezo.
Lengo kuu la Bonanza hili ni kusaidia kuzuia magonjwa yasiyoambukiza miongoni mwa watumishi wa umma, kuboresha afya zao na kuwaandaa kwa ushiriki bora katika mashindano mbalimbali ya kitaifa kama vile Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI), Kombe la Mei Mosi, Michezo ya Majeshi (BAMMATA) michezo ya SHIMMUTA na michezo ya Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA).
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bonanza hilo, Charles Shija, amesema mbali na faida za kiafya, Bonanza limekuwa jukwaa la kuimarisha mahusiano na mshikamano baina ya taasisi mbalimbali za umma, jambo linalochochea ushirikiano wa kikazi.
Naye Hamida Juma Mwisa, mtumishi kutoka Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), amesema ushiriki wao kwenye Bonanza hilo umekuwa na manufaa makubwa kiafya kutokana na aina ya kazi wanazofanya ambazo mara nyingi ni za kukaa ofisini kwa muda mrefu.
Bonanza la Mahala Pa Kazi linaendeshwa chini ya kaulimbiu isemayo: "Michezo kwa Afya."
No comments:
Post a Comment