
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha kwa asilimia 100 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025 /2026 baada ya wabunge wote kuyapatisha kwa kura ya ndiyo.
Siku ya Alhamisi Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, aliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha jumla ya Shilingi trilioni 1.016 kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti hiyo, ambapo asilimia kubwa ya fedha hizo zitatumika kwenye miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha bajeti hiyo Alhamisi, Aweso alieleza kuwa kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 73.77 ni kwa matumizi ya kawaida, ambapo Shilingi bilioni 18.08 ni kwa matumizi mengineyo (OC), Shilingi bilioni 55.69 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Wizara, RUWASA, Chuo cha Maji na Mfuko wa Taifa wa Maji.
Shilingi bilioni 943.11 zimetengwa kwa ajili ya maendeleo, ambapo Shilingi bilioni 340.46 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 602.65 ni fedha kutoka nje ya nchi.
Waziri Aweso alisema bajeti hiyo inalenga kuendeleza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini, ambayo tayari imeanza kuzaa matunda kwa wananchi wengi vijijini na mijini. Alisisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana yanaendana moja kwa moja na uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Mheshimiwa Spika, mafanikio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwenye Sekta ya Maji ni sawa na taa za hazard, hata ukizima gari, zinabaki zinawaka. Ndio maana Sekta ya Maji tunasema, ng’ara Samia ng’ara,” amesema Aweso.
Amesema bajeti hiyo itaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji, kuboresha huduma kwa wananchi, pamoja na kuimarisha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji.

No comments:
Post a Comment