IDADI YA MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 124 – WAZIRI NDEJEMBI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 23, 2025

IDADI YA MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 124 – WAZIRI NDEJEMBI



Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi,akizungumza na waandishi wa habari leo Mei23,2025 jijiniDodoma, kuhusu mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Na Okuly Julius _ DODOMA


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi,amesema idadi ya vijiji vilivyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi imeongezeka kutoka 2,088 mwaka 2021 hadi kufikia 4,679 kufikia Mei 2025.

Amesema ni sawa na ongezeko la vijiji 2,591, ambalo ni sawa na asilimia 124, jambo linalothibitisha jitihada za serikali katika kuhakikisha usimamizi bora wa rasilimali ardhi nchini.

Ndejembi ameyasema hayo leo Mei 23,2025 jijini Dodoma, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Serikali imeweka mkazo mkubwa kwenye upangaji wa matumizi ya ardhi ili kuhakikisha matumizi endelevu na yenye tija kwa wananchi. Mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano wa karibu kati ya wizara, halmashauri, wadau wa maendeleo na wananchi kwa ujumla,” alisema Mhe. Ndejembi.

Amebainisha kuwa Wizara hiyo imeendelea kushiriki kikamilifu katika miradi mikubwa ya kimkakati ya kitaifa kwa kupanga na kupima maeneo ya utekelezaji wa miradi hiyo. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) lenye urefu wa kilomita 1,146 kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga, pamoja na ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR).

Aidha, akizungumzia maendeleo katika sekta ya ujenzi wa makazi na biashara, Waziri Ndejembi amesema kuwa mradi wa Morocco Square jijini Dar es Salaam umefanikiwa kukamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 137, ambapo nyumba zote 100 zimeuzwa na maeneo ya biashara pamoja na ofisi tayari yamepangishwa. Pia, ujenzi wa mradi wa Kawe 711 umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2025/26. Mradi huo unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 169.

Katika hatua nyingine, Wizara imekamilisha marekebisho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 na kuanzisha toleo jipya la mwaka 2023 ambalo limesainiwa na kuzinduliwa rasmi na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 17 Machi 2025. Sera hiyo inalenga kuweka mfumo madhubuti wa umiliki wa ardhi, kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa ardhi, pamoja na kuwezesha matumizi ya ardhi kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Pamoja na hayo, Serikali imeanzisha Kitengo cha Milki ili kusimamia kikamilifu sekta ya milki na inaendelea na mchakato wa kutunga sheria ya Milki itakayounda Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Milki (Real Estate Regulatory Authority), kwa lengo la kuhakikisha sekta hiyo inasimamiwa kitaalamu, kwa uwazi na kwa tija kwa taifa.

Kwa upande wa upangaji na upimaji wa ardhi, Waziri Ndejembi alieleza kuwa Wizara imepokea jumla ya shilingi bilioni 64.5 kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika halmashauri 131 nchini. Kati ya hizo, shilingi bilioni 50 zimekopeshwa halmashauri 57 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Ardhi (PDRF), ambapo hadi sasa jumla ya viwanja 556,191 vimepimwa.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) umewezesha uhakiki wa mipaka ya vijiji 871 na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa vijiji 846, huku vipande vya ardhi 583,734 vikihakikiwa na kupandishwa katika mfumo wa kielektroniki wa e-Ardhi. Pia, hati za hakimiliki za kimila zipatazo 318,868 zimesajiliwa katika vijiji 236 vilivyopo katika wilaya sita, zikiwemo Songwe, Chamwino, Mufindi, Mbinga, Maswa na Tanganyika.

Kwa mujibu wa Waziri Ndejembi, mafanikio hayo yote ni ushahidi wa azma ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha sekta ya ardhi nchini, kuondoa migogoro ya ardhi, na kuwezesha wananchi kutumia ardhi yao kama mtaji wa maendeleo.

“Tunatoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza mipango hii ya kimkakati ili kuhakikisha miji na vijiji vyetu vinakua kwa mpangilio, vinavutia wawekezaji na vinawezesha maisha bora kwa wananchi,” alisisitiza Waziri.

No comments:

Post a Comment