IDADI YA WATALII WA KIMATAIFA YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 132.1 - BALOZI DKT. CHANA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, May 19, 2025

IDADI YA WATALII WA KIMATAIFA YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 132.1 - BALOZI DKT. CHANA


Na Okuly Julius DODOMA 


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, amesema kuwa idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 132.1, kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 2,141,895 mwaka 2024.

Aidha, amesema kuwa idadi ya watalii wa ndani waliotembelea vivutio vya utalii nchini imeongezeka kwa asilimia 307.9, kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi 3,218,352 mwaka 2024. Kwa pamoja, idadi ya watalii wote imefikia 5,360,247, sawa na asilimia 107.2 ya lengo la watalii 5,000,000 lililoainishwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2020.

Wazira Chana ameyasema hayo leo Mei 19,2025 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025-2026.


Waziri Chana amesema Tanzania imeendelea kuongoza Afrika na duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyamapori, ikiwa ni pamoja na simba wapatao 17,000, nyati 225,000 na chui 24,000. Kwa upande wa faru weusi, idadi yao imeongezeka kutoka 163 mwaka 2021 hadi 263 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 61. Vilevile, matukio ya ujangili wa tembo yamepungua kwa takriban asilimia 90.

Akizungumzia mafanikio ya kimataifa, Waziri Chana amesema Tanzania imeendelea kung’ara kwa kushinda Tuzo saba (7) za Kimataifa za World Travel Awards (WTA) zinazotolewa na taasisi ya World Luxury Media Group Limited ya Uingereza, kutokana na ubora wa vivutio na huduma za utalii.

Aidha, eneo la Hifadhi ya Ngorongoro limerejeshewa hadhi yake kama Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro Lengai (UNESCO Global Geopark) mwezi Desemba 2024, baada ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha uhifadhi, kutangaza urithi wa jiolojia na kufuata miongozo ya UNESCO.

Katika kutambua mchango wa wadau wa utalii na uhifadhi, Waziri amesema Wizara imezindua The Serengeti Awards Desemba 2024 Jijini Arusha. Tuzo hizo zimewatuza viongozi mashuhuri akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (Tuzo ya Kiongozi Mwenye Maono), Mhe. Zakia Meghji na familia ya wachimbaji maarufu wa zamadamu, Louis na Mary Leakey. Tuzo hizo zitatolewa kila mwaka ili kuhamasisha uendelezaji wa sekta hiyo.

Akizungumzia ushawishi wa filamu katika utalii, Waziri amesema kuwa mbali na Royal Tour, Rais Samia pamoja na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi walishiriki katika filamu Amazing Tanzania na mwigizaji nyota wa China, Jin Dong. Filamu hiyo, iliyozinduliwa Mei 2024 Beijing na baadaye Novemba 2024 Dar es Salaam, imechangia ongezeko la watalii kutoka China kutoka 45,463 mwaka 2023 hadi 71,140 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 56.5. Filamu hiyo pia ilivutia kipindi maarufu cha Divas Hit the Road ambacho kilioneshwa na kutazamwa na watu takriban bilioni 1.2 ndani ya China na nchi jirani.

Waziri Chana amesema kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa uthubutu na weledi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuwataka Watanzania waendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kuiongoza nchi kwa ujasiri, maridhiano na maendeleo.

No comments:

Post a Comment