
Na Mwandishi _ Dodoma
Kampuni ya Mamba Minerals Ltd yenye Leseni ya uchimbaji Madini adimu (Rate Earth Elements) imesema itaanza ujenzi rasmi wa Mgodi huo Disemba,2025 na uzalishaji wa kwanza kufanyika mwisho wa mwaka 2026.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma wakati wa kikao kati ya Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde na Viongozi wa Kampuni za Mamba Minerals na Shenghe Ltd.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Mwenyekiti wa Kampuni ya Mamba Minerals Ndg.Russell Scrimshaw amesema Kampuni hiyo imeitikia wito wa serikali wa kuhakikisha uzalishaji wa madini unaanza mapema iwezekanavyo kamba ambavyo Waziri wa Madini amesisitiza na hivyo kwa kushirikiana na wabia wenza Kampuni ya Shenghe watahakikisha ujenzi wa mgodi unaanza mapema mwezi Disemba 2025 na uzalishaji wa kwanza kufanyika mwishoni mwa mwaka 2026.
Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Shenghe Ndg. Quangan Wang amesema Ujenzi wa mgodi huo pia utaenda sambamba na ujenzi wa Kiwanda cha kuchenjua na kusafisha madini hayo pamoja na ujenzi wa Mtambo wa kuzalisha umeme wa kuanzia megawati 10-12 kwa matumizi ya mgodi na jamii inayozunguka mradi.
Madini adimu haya hutumika kwenye kutengeneza vifaa vya kieletroniki,vifaa vya uzalishaji umeme kutumia upepo,Mota za magari ya umeme na Vifaa vya hospitali.
Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amepongeza hatua ya Kampuni hiyo kuzingatia maelekezo ya serikali ya kuanza uendelezaji wa mgodi wa madini adimu kwa uharaka na kuendelea kusisitiza kwamba wamiliki wote wa Leseni za kati na Leseni kubwa kuhakikisha wanaanza shughuli za uchimbaji wa madini ndani ya miezi 18 ambayo imetamkwa kwenye Sheria ya Madini Sura ya 123.




No comments:
Post a Comment