KUELEKEA BAJETI YA WIZARA YA ELIMU, WANANCHI MWANZA NA DODOMA WAIPA HEKO SERA MPYA YA ELIMU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, May 11, 2025

KUELEKEA BAJETI YA WIZARA YA ELIMU, WANANCHI MWANZA NA DODOMA WAIPA HEKO SERA MPYA YA ELIMU


Mtaala mpya wa elimu umeanza kutumika , ukiwa na lengo la kuimarisha ujuzi, stadi, ubunifu, na maarifa kwa wanafunzi.

Mtaala huu unasisitiza zaidi mafunzo kwa vitendo (competency-based curriculum) badala ya mfumo wa zamani wa kukariri, hivyo kuwawezesha wanafunzi kuwa wabunifu, wenye stadi za maisha na maandalizi bora kwa ajili ya ajira au kujiajiri.


Vipengele Muhimu vya Mtaala Mpya


Marekebisho haya yanahusisha elimu ya awali hadi sekondari, ambapo mitaala imeelekeza nguvu katika kukuza stadi za maisha, ubunifu, maadili, na matumizi ya teknolojia. Mtaala huu mpya umebeba dhima ya kuandaa wanafunzi kwa mahitaji ya sasa ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia.


Maoni ya Wananchi Kuhusu Sera Mpya ya Elimu


Kuelekea bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itakayowasilishwa bungeni jijini Dodoma tarehe 12 na 13 Mei 2025, wananchi wa mikoa ya Mwanza na Dodoma wamepongeza mtaala mpya wa elimu, wakisema kuwa utaleta mabadiliko makubwa katika elimu na kusaidia vijana kuwa na kiwango bora cha elimu pamoja na uwezo wa kuchangamkia fursa mbalimbali.

Wakazi wa Mwanza, akiwemo Abdallah Rashid, Tonny Aliphonce na Yusuph Yahaya, wameeleza kuwa sera mpya ya elimu ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya taifa. Wamesema kuwa inalenga kuboresha ubora wa elimu ili iendane na mahitaji ya sasa ya jamii, uchumi na teknolojia.

Wananchi hao wamebainisha kuwa maeneo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele ni pamoja na elimu ya ufundi na ujasiriamali, ili kuongeza ujuzi na maarifa ya vitendo kwa vijana. Wamesema sera hii itawawezesha vijana kuwa tayari kwa soko la ajira na kujitegemea kiuchumi.

Kwa upande wao, wakazi wa Dodoma wakiwemo Hassan Mkumba, Jackson Tegemeo na Elieza Mgonja, wamesema kuwa sera mpya inasisitiza malezi ya kiutu, uzalendo na nidhamu miongoni mwa wanafunzi, jambo ambalo linachangia kujenga jamii yenye mshikamano na maadili mema.


TEHAMA na Elimu Jumuishi


Wananchi hao pia wamepongeza hatua ya sera hii kuweka mkazo kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), pamoja na kuhakikisha watoto wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum, wanapata fursa sawa ya elimu bora. Aidha, wamepongeza juhudi za kuhakikisha watoto wote wanaandikishwa shule, na kuboreshwa kwa miundombinu ya shule hadi maeneo ya vijijini.

Sera hii ndiyo msingi wa mabadiliko ya mtaala mpya wa elimu, unaoendana na mazingira ya sasa, teknolojia, na mahitaji ya dunia ya leo. Pia imeweka mikakati ya kuongeza idadi ya walimu, kuwajengea uwezo na kuboresha mazingira ya shule pamoja na vifaa vya kujifunzia.

Wananchi wana matumaini kuwa kupitia bajeti ijayo ya Wizara ya Elimu, utekelezaji wa sera mpya utaimarishwa zaidi kwa manufaa ya kizazi kijacho na maendeleo ya taifa kwa ujumla.




No comments:

Post a Comment