MAKATIBU TAWALA WASAIDIZI WAPEWA SOMO USIMAMIZI WA MIRADI NA USULUHISHI WA AKAUNTI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, May 19, 2025

MAKATIBU TAWALA WASAIDIZI WAPEWA SOMO USIMAMIZI WA MIRADI NA USULUHISHI WA AKAUNTI



Angela Msimbira, PWANI


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sospeter Mtwale, amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa kuhakikisha wanazisimamia Halmashauri zote kufanya usuluhishi wa akaunti za kibenki, hususani tunapoelekea mwishoni mwa mwaka wa fedha wa Serikali.

Akizungumza leo Mei 19, 2025 katika ufunguzi wa Mafunzo ya Uongozi kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa yanayofanyika mkoani Pwani, Mtwale amesema bado kuna baadhi ya Halmashauri ambazo zimekuwa na akaunti ambazo hazijafanyiwa usuluhishi kwa muda mrefu, hali inayokwamisha uwajibikaji na utawala bora wa fedha za umma.

“Mikoa ni taasisi wezeshi. Hakikisheni kuwa mnazisimamia Halmashauri zilizo chini yenu kuhakikisha usuluhishi wa akaunti unafanyika kikamilifu kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha,” amesisitiza.

Aidha, amewakumbusha viongozi hao wajibu wao wa msingi katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika maeneo mbalimbali ya mikoa, akiwataka kuhakikisha miradi hiyo inakidhi viwango na kuendana na thamani ya fedha inayotolewa na serikali.

Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa Makatibu Tawala Wasaidizi kushirikiana kikamilifu katika kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa wakati na kwa weledi, ili kupunguza idadi ya hoja za ukaguzi zinazojitokeza kila mwaka.

“Serikali ina sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya usimamizi wa rasilimali watu na fedha. Ikiwa viongozi mtaisimamia kikamilifu, hoja za ukaguzi zitapungua kwa kiasi kikubwa. Nendeni mkalisimamie hili kwa umakini mkubwa,” amesisitiza.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa serikali kupitia Taasisi ya Uongozi na Ofisi ya Rais – TAMISEMI wa kuimarisha uwezo wa viongozi wa ngazi ya mikoa katika kusimamia utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.




No comments:

Post a Comment