MAVUNDE ATANGAZA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO JIPYA LA MTUMBA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 15, 2025

MAVUNDE ATANGAZA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO JIPYA LA MTUMBA



Na Okuly Julius DODOMA


Mbunge wa Dodoma Mjini ambaye pia ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ametangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo jipya la Mtumba iwapo atapitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza jana katika mkutano maalum wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Dodoma, Mavunde alisema amefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina, kusikiliza na kupima hoja mbalimbali kutoka kwa wananchi na viongozi wa chama.

“Natangaza rasmi kuwa katika uchaguzi ujao nitagombea Jimbo la Mtumba,” alisema Mavunde huku akibainisha kuwa jimbo hilo lina changamoto nyingi zinazogusa maisha ya wananchi, hivyo linahitaji kiongozi makini na mwenye maono.

Alisema Jimbo hilo jipya linajumuisha maeneo ya kimkakati kama ujenzi wa Hombolo Satellite City na Ihumwa Yard, miradi ambayo inahitaji usimamizi wa karibu ili kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo.

“Ni jimbo jipya lenye changamoto nyingi na wananchi wengi wenye kiu ya maendeleo. Nikipitishwa kuwa mgombea, nitafanya kampeni katika maeneo yote, na nikipewa dhamana nitakuwa mbunge wa wote,” alisisitiza Mavunde.

Kabla ya kutangaza uamuzi wake, Mavunde alisifu juhudi kubwa zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo ndani ya Jimbo la Dodoma Mjini kupitia miradi mikubwa ya kimkakati, hali iliyofanya mkoa huo kung'aa kitaifa.

“Nitaendelea kuwa Mbunge wa Dodoma Mjini hadi Juni 27, 2025. Nawashukuru wananchi kwa kunipa heshima ya kuwa mwakilishi wao,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa kawaida historia ya Jimbo la Dodoma Mjini imekuwa ikimpa mbunge muda wa miaka mitano tu, isipokuwa Mbunge Sagafu ambaye alihudumu kwa miaka 10. “Wananipa heshima kubwa sana. Naitambua dhamana hiyo na naichukulia kwa uzito,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma, Sophia Chibaba, alisema mgawanyo wa Jimbo la Dodoma ni hatua muhimu ya kuimarisha ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kwa kuzingatia ukubwa wake unaojumuisha kata 41 na mitaa 222.

No comments:

Post a Comment