Na Okuly Julius _ DODOMA
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini , ambaye pia ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amegawa matofali 41,000 na mifuko ya saruji tani 102 (sawa na mifuko 2,050) kwa kata zote 41 za jimbo hilo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia Mfuko wa Jimbo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mavunde alisema vifaa hivyo vimetolewa kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi ya elimu na afya katika kata hizo. Alieleza kuwa Mfuko wa Jimbo uko katika hali nzuri na kwa sasa umekuwa ukipokea Sh milioni 93 kila mwaka.
Akiainisha baadhi ya miradi iliyotekelezwa, Mavunde alisema miradi ya afya na elimu imepewa kipaumbele, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Miongoni mwa vifaa vilivyotolewa kwa wananchi ni pamoja na mashine za kutotolesha vifaranga, mashine za kutengeneza juisi, pamoja na mashine za kunyonyolea kuku katika soko la Majengo.
“Kama tulivyoahidi, kila mwaka tutakuwa tukitoa mashine ya kusafishia mafuta ya alizeti kwa kata ya Ipagala. Hilo ni moja ya mafanikio mengi tuliyopata,” alisema Mavunde.
Hata hivyo, alieleza kusikitishwa na tabia ya baadhi ya maeneo kutozitumia saruji kwa wakati hadi inaganda. Alitoa rai kwa viongozi wa kata kuhakikisha vifaa vinatumika kama ilivyokusudiwa.
Mavunde pia alitangaza mpango wa kuchimba visima 25 katika kipindi cha miezi miwili ijayo katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, ikiwemo Chididimo na Nkulabi, ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama.
Akizungumzia miradi ya kitaifa, Mavunde alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya maendeleo, ikiwemo utoaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa Mji wa Serikali jijini Dodoma. Alibainisha kuwa mradi huo umechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa biashara na ajira kwa wakazi wa Dodoma.
Aidha, alieleza kuwa Rais Samia ameridhia ujenzi wa barabara ya Ihumwa kwa kiwango cha lami na mchakato wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kuelekea Hombolo umeanza. Pia, Rais ametoa fedha kwa ajili ya kuchimba na kujenga upya Bwawa la Hombolo ili kuhakikisha maji yanafika kwenye mashamba ya wakulima.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, alimshukuru Rais Samia kwa kupeleka gari jipya kwa ajili ya Mkuu wa Wilaya, pamoja na kujenga ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma na ofisi tatu kati ya nne za maofisa Tarafa.
“Tukiendelea kumshukuru Rais Samia, wengine hudhani ni kujipendekeza. Lakini ukweli ni kwamba wilaya yetu haijawahi kuwa na ofisi kamili, sasa tunaiona dhamira ya dhati ya maendeleo,” alisema Shekimweri.
Naye Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fadhili Chibago, alisema Mbunge Mavunde ameweka kipaumbele kwenye miradi ya elimu na afya, jambo linalogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.
“Mbunge wetu anafanya kazi kubwa, na tunampongeza kwa moyo wake wa kujitoa kuhudumia wananchi,” alisema Chibago.
No comments:
Post a Comment