Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameiagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuongeza juhudi za kusajili wataalam wa kada ya mafundi sanifu na kuwajengea uwezo, kwani idadi iliyopo sasa hailingani na ile wanaostahili kusajiliwa.
Waziri Ulega alitoa agizo hilo leo tarehe 22 Mei, 2025 mkoani Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya saba ya siku ya mafundi sanifu ambao ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali.
Mkutano huo ulihudhuriwa na mafundi sanifu zaidi ya 800 ukiwa na mada isemayo 'Muundo wa utumishi kwa kada ya mafundi sanifu katika utumishi wa umma na sekta binafsi’.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Waziri Ulega pia aliiagiza bodi hiyo ishirikiane na vyuo vinavyozalisha wataalam hao ili kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wanaosomea fani hizo.
Vilevile, Waziri Ulega aliiagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuongeza idadi ya usajili wa mafundi sanifu wa uhandisi wenye sifa stahiki za kitaaluma na ambao wana uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la ajira na katika miradi ya kimkakati hapa nchini.
Pia, aliiagiza kuandaa mkakati wa kutambua mafundi sanifu walio pata ujuzi kwa njia isiyo rasmi ili waajirike katika mazingira ya mfumo rasmi pamoja na kuharakisha mpango wa mapitio ya muundo wa mafundi sanifu kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na sekta nyingine.
Waziri Ulega alisema maagizo hayo aliyoyatoa pamoja na maazimio ya mkutano huo yawasilishwe Wizara ya Ujenzi kabla ya Juni 30 mwaka huu.
"Nimembiwa kuwa Bodi ya Usajili wa Wahandisi imesajili mafundi sanifu zaidi kidogo ya elfu tatu hadi sasa. Idadi hii ni ndogo ukilinganisha na idadi ya wale wanaostahili kusajili pamoja mahitaji ya mafundi sanifu waliosajiliwa hapa nchini. Naiagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi kuongeza juhudi ya kusajili Wataalam wa kada ya Mafundi Sanifu na kuwajengea uwezo”, alisema Waziri Ulega.
Kadhalika, Waziri Ulega alisema katika jitihada za kukuza uchumi Serikali itaendelea kuimarisha na kuboresha mazingira ya kibiashara na ya uwekezaji katika viwanda pamoja na kuhamasisha wadau kujenga viwanda vipya hususan vile vinavyotumia malighafi za ndani.
Hivyo, aliwataka mafundi sanifu hao kuchapa kazi, kufanya kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa pamoja na kukamilisha miradi yote vizuri kwa muda uliopangwa na kwa thamani iliyo halisi.
Waziri Ulega alisema Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na bodi za kitaaluma ikiwemo ERB na AQRB wameanza zoezi la kupitia upya muundo wa utumishi na maslahi ya wataalam wa ujenzi.
Alisema Serikali inafahamu changamoto wanazopita mafundi sanifu pamoja na kupanda vyeo kwa njia ya mserereko hususani fundi sanifu aliyefikia cheo cha afisa mkuu akiwa mhandisi asianze mwanzo.
"Nafahamu viongozi waandamizi kutoka Ofisi ya Rais Utumishi wako hapa, ninawasihi, kuweni huru kutoa maoni na mapendekezo yenu, lakini mfanye hivyo kwa lugha murua na staha na serikali chini ya Jemedari wetu Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tutayafanyia kazi”, alisema Waziri Ulega.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mwajuma Waziri aliwataka mafundi sanifu kushikamana kwa upendo ili waweze kutimiza malengo yao waliyoyaweka.
Alisema mafundi sanifu ni kada muhimu inayotegemewa katika kuhakikisha michoro ya miradi inatekelezeka.
No comments:
Post a Comment