MWENYEKITI WA TUME YA MADINI AONGOZA KIKAO CHA KAMISHENI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 14, 2025

MWENYEKITI WA TUME YA MADINI AONGOZA KIKAO CHA KAMISHENI



Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Reuben Lekashingo, ameongoza kikao muhimu cha Kamisheni ya Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma.

Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha miezi mitatu, sambamba na kuweka mikakati ya kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuwa mhimili wa ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kikao hicho kilichohusisha Makamishna wa Tume na menejimenti, kiliweka mikakati mipya ya kuboresha usimamizi wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini, ukusanyaji wa maduhuli, na masoko ya madini, pamoja na kudhibiti utoroshaji wa madini ili kuongeza mchango wa sekta hii kwenye Pato la Taifa.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwake, Tume ya Madini imepiga hatua kubwa ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi katika mikoa 30 ya Tanzania Bara na ofisi 13 za Maafisa Migodi Wakazi kwa migodi mikubwa na baadhi ya migodi ya kati.

Pia, masoko 43 ya madini na vituo 109 vya ununuzi wa madini vimeanzishwa, huku mifumo thabiti ya kielektroniki kwa ukusanyaji wa mapato na utoaji wa leseni ikiwa imeimarishwa.

Mhandisi Lwamo aliongeza kuwa, mafanikio mengine ni pamoja na maboresho ya huduma za maabara kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini, pamoja na ushirikiano wa kimkakati na taasisi nyingine za serikali. Pia, kasi ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali imeendelea kukua, huku sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia sekta ya madini ikiendelea kuboreshwa ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji.

Alisisitiza kuwa kaguzi za mara kwa mara zimekuwa zikifanyika kwenye migodi ya uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa, pamoja na ukaguzi wa stoo na masanduku ya baruti.


Sambamba na hayo, elimu kuhusu usalama, afya na mazingira inaendelea kutolewa kwa wachimbaji wa madini ili kuhakikisha shughuli zao zinafanyika kwa kuzingatia usalama wa jamii na mazingira.

Kwa upande wake, Dkt. JR Lekashingo aliipongeza Tume ya Madini kwa kazi nzuri kwenye ukusanyaji wa maduhuli, usimamizi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi vilivyoanzishwa nchini, pamoja na juhudi za kuimarisha usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta hii muhimu.

Alisisitiza kuwa elimu kuhusu Sheria ya Madini na kanuni zake inapaswa kuendelea kutolewa kwa wadau kupitia ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa mikoa.

Katika kikao hicho, changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Madini zilijadiliwa kwa kina, huku mikakati kupitia Kamati za Ufundi, Rasilimaliwatu, Fedha na Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ikiwekwa ili kuhakikisha wachimbaji wanajipatia kipato katika mazingira rafiki na yenye tija kwa uchumi wa taifa.

Kwa taarifa zaidi kuhusu shughuli za Tume ya Madini, tafadhali tembelea tovuti yetu au ofisi zetu za Maafisa Madini Wakazi katika mikoa yote ya Tanzania Bara.







No comments:

Post a Comment