
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi) lenye urefu wa kilometa 3 na barabara zake unganishi zenye urefu wa kilometa 1.66 utakaofanyika tarehe 19 Juni, mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa leo tarehe 19 Mei, 2025 wakati alipokagua daraja hilo ambalo limekamilika kujengwa na litakuwa daraja refu zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

"Jitayarisheni kwa wingi kumpokea kiongozi wetu mkuu atakapokuja kulifungua daraja hili Juni 19, 2025 ", amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameeleza kuwa Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa Daraja hilo linalopita juu ya maji kwa kutumia fedha za ndani ikiwa ni jambo la kihistoria kwa nchi yetu.
Ameongeza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 700 zimetumika katika ujenzi wa daraja hilo linalounganisha mji wa Kigongo na Busisi katika Ziwa Victoria ambalo ni la tatu kwa ukubwa duniani.

Aidha, Waziri Ulega amewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Sengerema kuwa Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara ya Segerema - Nyehunge (km 54.5) na Kamanga - Sengerema (km 32) kwa kiwango cha lami ili ziweze kuifungua Wilaya hiyo na kuchochea uchumi.



No comments:
Post a Comment