
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia (PPPC), David Kafulila, na Mwenyekiti wa REDET, Prof. Rwekaza Mukandala.
Na Mwandishi Wetu _ Dar es Salaam
Serikali inatarajiwa kukabiliana na hoja za wanazuoni na sekta binafsi kesho kuhusu dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), mwenendo wa uchumi chini ya Awamu ya 6 na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia (PPPC) David Kafulila, mjadala huo wa wazi utafanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Kituo cha PPPC kitafanya kongamano kwa kushirikiana na Taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) ambayo iko chini ya UDSM.
Mada kuu ya kongamano ni: Dola, Masoko na Uhamasishaji wa Mitaji: Nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi Kufikia Malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
Kafulila atafanya wasilisho kuhusu Dhana ya PPP na Nafasi yake Kuelekea Dira ya Taifa 2050 na Mwenyekiti wa REDET, Prof. Rwekaza Mukandala, ataongoza kongamano kama moderator.
Kongamano litafanyika katika Ukumbi wa Maktaba Mpya, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jumanne tarehe 27 Mei 2025 kuanzia saa 3:00 asubuhi mpaka saa 6:00 mchana.
Maafisa waandamizi wa serikali, wakuu wa makampuni ya sekta binafsi, wanazuoni na wawakilishi wa kada nyingine mbalimbali wanatarajiwa kushiriki kwenye mjadala wa wazi utakaorushwa mubashara na vituo kadhaa vya televisheni.
"Wananchi wote wanakaribishwa kuhudhuria kongamano hili la wazi ili waweze kushiriki kwenye mjadala kuhusu dhana ya PPP na nafasi yake kwenye kutekeleza Dira ya Taifa 2050," Kafulila amesema.
"Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) una nafasi kubwa kwenye mwelekeo mpya wa uchumi na maendeleo ya Tanzania."
Kituo cha PPPC kinasimamia jumla ya miradi 84 ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Miradi hiyo ipo kwenye sekta za usafirishaji, nishati, miundombinu na maeneo mengine.
Baadhi ya miradi hiyo ni Barabara ya waendao haraka (Express way) ya Kibaha–Chalinze -Morogoro (205km), na ile ya Isongole-Tunduma (210km) ambazo zikijengwa njia nne za barabara (epxress way), zinaweza kugharimu karibu dola za Marekani Bilioni 1.6.
Mradi wa barabara kwa ajili ya kupunguza foleni katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Outer ring roads) nao ni miongoni mwa miradi ya kutekelezwa kwa ubia wa PPP.
No comments:
Post a Comment