ULEGA ASISITIZA UBORA NA KASI KATIKA MIRADI YA MIUNDOMBINU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 21, 2025

ULEGA ASISITIZA UBORA NA KASI KATIKA MIRADI YA MIUNDOMBINU



Na Okuly Julius _ DODOMA


Waziri wa Ujenzi Mhe Abdallah Ulega amewataka watendaji wa wizara hiyo kuhakikisha wanawasimamia kikamilifu wakandarasi kukamilisha miradi kwa wakati na kuzingatia ubora kwani serikali haipo tayari kuendelea kuwaongezea muda wakandarasi ambao wamechelewesha miradi bila sababu za msingi.

Waziri ulega ametoa kauli hiyo jijini Dodoma mara baada ya Ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko nje ya jiji la Dodoma (DODOMA OUTER RING ROAD) yenye urefu (km 112.3) ambapo kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 85 ya utekelezaji wake na mradi wa Ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Msalato .

“Nimekagua na nimeridhishwa na hatua zilizofikiwa katika awamu zote mbili na malengo ya Serikali ni kuwa mradi huu ukamilike kwa wakati na nimeelekeza wataalam kutoka TANROADS hadi kufikia mwezi Juni wawe wamefika asilimia 90”, amesisitiza Ulega.

Kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika jiji la Dodoma Waziri Ulega amesema kuwa Serikali inatarajia kujenga barabara ya njia nne na sita kuanzia Chamwino Ikulu hadi katikati ya jiji hilo ambapo kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za manunuzi za kumpata mkandarasi wa kujenga mradi huo.

Ameongeza kuwa katika eneo la Ihumwa Serikali ina mpango wa kujenga barabara ya kisasa ya njia za kupishana (interchange), ili kuruhusu magari kupita katika mji wa Serikali wa Magufuli na yaendayo mjini bila kuwa na kizuizi chochote.

Vilevile, Waziri Ulega amezungumzia umuhimu wa Taasisi za TANROADS, TRC na TPA kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuwezesha mradi huo wa kimkakati kukamilika kwa wakati.

Aidha , akiwa katika ziara hiyo Ulega pia alifafanua kuhusu ujenzi wa miundombinu ya barabara za juu (flyovers) katika eneo la Morocco na Mwenge jijini Dar es salaam ambapo amesisitiza kuwa miradi hiyo ipo kwenye mpango mzuri na hatua iliyofikiwa sasa ni kuwa Wizara inaendelea kukamilisha taratibu za kitaalam ili kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.

“Nitumie fursa hii kuwaambia watanzania kwamba bado Serikali inayo mpango wa kuzijenga Flyover za Mwenge na Morocco na hatua iliyopo wataalam wameniambia wanakamilisha taratibu na wafadhili wa mradi JICA hadi kufikia mwezi Julai fedha za mkopo zitakuwa zishasainiwa ”, amesisitiza Ulega.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Aloyce Matei amesema kuwa hadi kufikia mwezi wa saba matarajio yao ni kwamba fedha za mradi wa ujenzi wa barabara za juu za Morocco na Mwenge zitasainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Naye, Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Japheson Nnko amemhakikishia Waziri Ulega kuwa watasimamia Makandarasi hao kuhakikisha mradi wa mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma unakamilika kwa ubora na wakati kama ilivyosainiwa kwenye mkataba.

Amebainisha kuwa mradi huo umegawanywa sehemu mbili ambapo Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) anayejenga sehemu ya Nala-Veyula-Mtumba-Ihumwa bandari kavu (km 52.3) anatarajiwa kukamilisha ifikapo mwezi Julai, 2025 na Mkandarasi Avic International anayejenga sehemu ya Ihumwa bandari kavu-Matumbulu-Nala (km 60) anatarajiwa kukamilisha ifikapo mwezi Agosti, 2025.


Katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Msalato ,Waziri Ulega ameielekeza TANROADS kushirikiana na TAA kuhakikisha ubora unazingatiwa kwani hitaji la watanzania ni kuona uwanja huo ambao utaufungua uchumi wa Dodoma na Nchi kwa ujumla unakamilika kwa wakati.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Abdul Mombokaleo ameeleza ni lini wanatarajia kufanya majaribio ya ndege katika Kiwanja hicho



No comments:

Post a Comment