WIZARA YA MADINI YAHAMIA RASMI MTUMBA DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 15, 2025

WIZARA YA MADINI YAHAMIA RASMI MTUMBA DODOMA


Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ametangaza rasmi kuwa Wizara ya Madini imehamia eneo la Mtumba jijini Dodoma, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa kuwaweka karibu na huduma zote muhimu.

Waziri Mavunde amesema kuwa uamuzi huo umetokana na dhamira ya Serikali kuhakikisha wananchi hawapati usumbufu wa kutafuta huduma katika maeneo tofauti tofauti.

“Kwa sasa, vitengo vyote vya wizara vitakuwa pamoja, na hii itapunguza adha iliyokuwa ikiwakumba wananchi kutokana na ufinyu wa nafasi,” amesema Mavunde.

Mradi huo mkubwa unaogharimu Shilingi bilioni 300 umeelezwa kuwa utawanufaisha wananchi wanaohitaji huduma, na pia kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa sekta ya madini na huduma nyingine zinazohusiana na shughuli za wizara hiyo.

Waziri Mavunde amewapongeza watumishi wa wizara kwa usimamizi mzuri wa mradi huo uliowezesha kukamilika kwa jengo hilo kwa wakati.

“Nawapongeza kwa moyo wa uzalendo na kazi nzuri mlioifanya hadi kufanikisha mradi huu muhimu,” amesema.

Amesisitiza kuwa licha ya wizara kuhamia Mtumba, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) itaendelea kubaki kwenye eneo lake la awali ili kuendelea kutoa huduma za kitaalamu.

“Hii ni hatua muhimu ya kutekeleza maagizo ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini. Mimi binafsi nimekamilisha ahadi yangu ya kuhamishia wizara Mtumba kama sehemu ya mageuzi ya utendaji katika sekta ya madini,” amesema.

Waziri amewataka watumishi wote wa Wizara ya Madini kuendelea kuwa na weledi, uwajibikaji na moyo wa kutoa huduma bora kwa Watanzania, akisisitiza kuwa jengo la kisasa pekee halitoshi bila huduma bora kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment