DKT. MSONDE : TUMIENI HUDUMA ZA WASANIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI KULETA TIJA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 25, 2025

DKT. MSONDE : TUMIENI HUDUMA ZA WASANIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI KULETA TIJA


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde amezungumzia umuhimu wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi nchini (AQRB), kujitangaza ili huduma zao zitumiwe na wananchi wengi.

Akifungua semina ya siku mbili ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kuhusu mafunzo endelevu jijini Dar es Salaam leo tarehe 25 Juni, 2025 Dkt. Msonde amesema Serikali itaendelea kuiunga mkono AQRB ili isimamie kikamilifu sekta hiyo na hivyo kuleta tija na ustawi kwa wananchi na sekta ya majenzi kwa ujumla.

"Kazi ya kuelimisha wananchi iwe endelevu ili wananchi wengi wajenge nyumba za kisasa na bora kwa gharama nafuu", amesema Dkt. Msonde.

Naibu Katibu Mkuu Msonde amehimiza matumizi ya TEHAMA katika sekta ya majenzi ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Amesema Serikali itaendelea kutumia wataalam wazawa katika miradi mingi hivyo waungane ili wapate fursa ya kupata miradi itakayo wawezesha kukuza ujuzi na uchumi wa wataalam na kampuni kwa ujumla.

"Tuwe na dhamira ya kujiendeleza kiujuzi, weledi, uadilifu na uzalendo ili kufikia malengo", amesisitiza Dkt. Msonde.

Ameitaka AQRB kufanya tafiti ili kupata wataalam na kuwasajili kwa wakati, kuendeleza programu za mafunzo ili kuendana na wakati, kushiriki miradi ya ndani na nje ya nchi na kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya majenzi nchini.

Naye, Kaimu Msajili AQRB Arch. Dkt. Daniel Matondo amesema semina hiyo ina lengo la kuwaweka wataalam wa majenzi pamoja kujadili na kubuni ufumbuzi utakaowezesha sekta ya majenzi kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Amesema mafunzo hayo yanayoongozwa na kauli mbiu kujenga utaalam endelevu viwango na mikakati yanakusudia kuhamasisha Serikali na jamii kutoa kipaumbele kwa fani za ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi kwa ustawi wa nchi.

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Wahandisi, Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi Zanzibar Arch. Yasir De Costa amezungumzia umuhimu wa wataalam hao Kutoka pande zote za Muungano kushirikiana na kusaini mikataba itakayowawezesha kufanyakazi kwa umoja na kunufaika na fursa zilizopo nchini.

Zaidi kampuni 491 na wataalam 1707 wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi wamesajiliwa na AQRB kufanya shughuli za majenzi nchini kote.

No comments:

Post a Comment