DUWASA YAWATAKA WANANCHI KUTOA TAARIFA MAPEMA WANAPOKUMBWA NA CHANGAMOTO YA HUDUMA ZA MAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 24, 2025

DUWASA YAWATAKA WANANCHI KUTOA TAARIFA MAPEMA WANAPOKUMBWA NA CHANGAMOTO YA HUDUMA ZA MAJI


Na Okuly Julius DODOMA 


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imewataka wananchi kutoa taarifa mapema pindi wanapokuwa na changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji, hasa katika siku ambazo wanapaswa kupata maji ili mafundi waweze kufika na kutatua tatizo.

Kauli hiyo imetolewa na Mhandisi wa DUWASA Peter Shemwelekwa wakati wa Mkutano wa Wananchi uliofanyika katika eneo la Mahungu kujadili changamoto ya maji na kutafuta suluhu.

“Ukiona hupati maji, tunakuomba utoe taarifa mapema. Usipofanya hivyo unapoteza haki yako ya kupata huduma ya maji" alisisitiza Mha. Shemwelekwa.

Aidha, amebainisha kuwa, kuna mikakati madhubuti ya kupunguza adha ya maji katika eneo la Mahungu na maeneo mengine ya Jiji la Dodoma kupitia Mradi wa Uchimbaji Visima Pembezoni mwa Jiji la Dodoma.

Mha. Shemwelekwa amesema kukamilika kwa Mradi wa Maji Awamu ya Pili wa Nzuguni kutasaidia kuongeza upatikanaji wa maji kwa kiasi kikubwa.

“Mradi huu utakapokamilika, maji yanayoelekezwa sasa katika maeneo ya Ilazo, Swaswa, Ipagala na Kisasa kutoka chanzo cha Maji Mzakwe yataelekezwa maeneo mengine, ikiwemo Tenki la Itega, ambalo ndilo linalosambaza maji katika eneo la Mahungu. Hii itapunguza sana adha ya maji,” alisema.


Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa Mahungu wameipongeza DUWASA kwa jitihada inazofanya na kuiomba kuongeza juhudi zaidi za kutafuta suluhisho la kudumu.

Wananchi hao wameishauri Mamlaka hiyo kuendelea kufanya utafiti wa kina katika eneo la Mahungu kwa ajili ya kuchimba visima, ili kuongeza vyanzo vya maji na kupunguza changamoto ya maji.

No comments:

Post a Comment