Chuo cha Uhasibu Arusha pamoja na Chuo cha Heriot-Watt University (UK) kupitia shule ya Biashara wamesaini makubaliano kuhusu tafiti.
Akizungumza katika utiaji saini wa makubaliano hayo, Mkuu wa Chuo Profesa, Eliamani Sedoyeka alieleza kuwa Chuo Kikuu cha Heriot Watt ni moja ya taasisi za juu zinazoheshimika duniani na ushirikiano huo ni muendelezo wa IAA kujitanua kimataifa ambayo pia ni ajenda ya serikali ya awamu ya sita.
Prof. Sedoyeka ametaja maeneo makubwa ya ushirikiano kuwa ni katika uendeshaji wa programu za pamoja, tafiti na kubadilishana uzoefu kati ya wahadhiri na wanafunzi. Haya yote ni kwa ajili ya kuboresha uzoefu wa kujifunza na kufundisha na sio tu kwa IAA bali pia kwa Heriot-Watt.
Naye Profesa ,Angus Laing ambaye ni Mkuu wa Kitivo cha Edinburgh Business School amesema chuo chao kimefurahi kuingia makubaliano na IAA na wanaamini ushirikiano huu utakuwa na manufaa kwa pande mbili.
Ameongeza kuwa wakati wakitafuta Chuo cha kushirikiana nacho Tanzania, IAA ilikuwa Chuo kilichopendekezwa hata kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza na wamegundua tunahistoria na maadili ya msingi (values) yanayofanana.
Profesa Angus Laing ameeleza kwa sasa IAA imeingia rasmi kwenye mtandao wao wa Vituo vyao vya kimataifa ambapo wanavituo vitano vilivyoko Uingereza (UK), Dubai na Malaysia.
Naye Dk,Mwamini Tulli ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo amepongeza taasis zote mbili na ameahidi kuwa Baraza la Uongozi linatoa ushirikiano katika kuhakikisha makubaliano hayo yanakuwa na kufanikiwa kwa manufaa ya taasisi husika lakini pia nchi zetu.
No comments:
Post a Comment