MAJALIWA AZINDUA MIFUMO YA KIELEKTRONI KUUNGANISHA TAASISI ZA SERIKALI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 23, 2025

MAJALIWA AZINDUA MIFUMO YA KIELEKTRONI KUUNGANISHA TAASISI ZA SERIKALI



Na Okuly Julius , Dodoma


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amezindua mifumo miwili ya kielektroni inayowezesha taasisi za serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa urahisi (GovESB), pamoja na kuwawezesha watumishi wa umma kuwekeza katika mfumo wa faida.

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dodoma wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma, ambapo Waziri Mkuu alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Majaliwa amesema uzinduzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia ya kuzitaka wizara na taasisi za umma kuhakikisha kuwa mifumo yao ya ndani inasomana, ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi serikalini.


“Naziagiza taasisi zote za serikali ambazo bado hazijajiunga na mfumo huu wa kitaifa kuhakikisha zimejiunga ifikapo Julai 30 mwaka huu. Hatutahitaji bajeti mpya kwa hili, wala hakuna gharama, hivyo kila taasisi ichukue hatua haraka,” amesema Mhe. Majaliwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, amesema hadi sasa taasisi 180 tayari zimejiunga na mifumo hiyo na taarifa zao zinaweza kusomwa na kushirikiana.

“Tunapiga hatua kubwa katika mageuzi ya kidijitali serikalini. Mifumo hii inaiwezesha serikali kuwa na uwazi, uwajibikaji na ufanisi zaidi katika utoaji wa huduma,” amesema Mhe. Simbachawene.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba, amesema mifumo hiyo miwili iliyozinduliwa ni Government Enterprise Service Bus (GovESB) kwa ajili ya mawasiliano ya kimfumo kati ya taasisi, na Mfumo wa Watumishi wa Umma (PSSSF Investment Platform) unaowawezesha watumishi kuwekeza kwa usalama na faida.

“Tunajivunia kuona Tanzania inakwenda sambamba na dunia katika matumizi ya TEHAMA serikalini. Hii inaleta mageuzi makubwa kwenye usimamizi wa taarifa na uwajibikaji,” amesema Mhandisi Ndomba.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2025 yamebeba kaulimbiu inayohimiza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utumishi wa umma kama njia ya kuongeza uwajibikaji, ufanisi, na huduma kwa wananchi.





No comments:

Post a Comment