
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk.Maduhu Kazi amewasisitiza wananchi kutembelea maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma kwa ajili ya kujifunza na kupata huduma.
Dk.Maduhu ameyasema hayo Juni 18, 2025 alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria ambapo aliipongeza pia Wizara hiyo kwa kutekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa vitendo.

“Maonyesho yanaendelea katika viwanja hivi na watumishi wamejipanga vema kutoa huduma kwa wananchi, niwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kujionea na kujifunza mambo mbalimbali,”alisema
Ameongeza kuwa:”Niwakumbushe kuwa wanaokuja hapa hawatoki kama walivyokuja kuna vitu wanajifunza ambavyo vitakuwa na msaada mkubwa katika maisha yao ya kila siku,”
Kwa upande wake Wakili wa Serikali Wizara ya Katiba na Sheria Nickson Maleko amesema, katika maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma Wizara hiyo imejipanga kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi na watumishi.
Amesema pia wanatoa namba ya Huduma kwa Mteja ambayo itawawezesha kuwasiliana na wizara moja kwa moja na kupatiwa huduma.
“Tunaendelea na maonyesho katika wiki ya utumishi wa umma ambapo katika banda letu kuna watalaamu mbalimbali ambao tumejipanga kuhakikisha tunatoa msaada wa kisheria kwa wananchi na watumishi watakaohitaji,”amesema.






No comments:
Post a Comment