NAIBU WAZIRI SANGU AWATAHADHARISHA WAGOMBEA KUJIEPUSHA NA RUSHWA MAJIMBONI, TAKUKURU IPO KAZINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 14, 2025

NAIBU WAZIRI SANGU AWATAHADHARISHA WAGOMBEA KUJIEPUSHA NA RUSHWA MAJIMBONI, TAKUKURU IPO KAZINI



Na. Lusungu Helela- NZEGA


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imejidhatiti kuhakikisha inadhibiti vitendo vya rushwa kabla, wakati na hata baada ya Uchaguzi Mkuu huku akiwaasa wagombea kujiepusha na vitendo vya rushwa huko majimboni kwani TAKUKURU ipo kazini.


Amesema kitendo cha Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kutoa jumla ya magari mapya 195 kwa ajili ya TAKUKURU ni uthibitisho tosha kuwa anachukia vitendo vya rushwa.

Mhe.Sangu ametoa kauli hiyo leo wakati akizindua Jengo la TAKUKURU Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora ambalo limegharimu kiasi cha Sh. Mil. 314.2 hadi kukamilika kwake.

Amesema TAKUKURU itawakamata wale wote watakaothubutu kutoa rushwa ya aina yeyote ile kwa lengo la kuwarubuni wapiga kura "Msikubali kurubuniwa na rushwa na atakayethubutu kufanya hivyo toeni taarifa kwa TAKUKURU" amesisitiza Mhe.Sangu

Amesema mbali ya kutoa magari hayo, katika kipindi chake cha uongozi Rais.Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kujenga jumla ofisi 25 katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini kwa lengo la kuwawezesha watumishi wa TAKUKURU kufanya kazi katika mazingira rafiki hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu

Aidha, Mhe. Sangu amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwa taasisi hiyo ambapo katika kipindi chake cha uongozi ameajiri watumishi wapya 1900 ikiwa ni nusu ya watumishi aliowakuta

Akizungumzia madhara ya kuchagua viongozi kwa njia ya rushwa, Mhe, Sangu amesema vitendo vya rushwa na makosa mengine yanayofanyika wakati wa uchaguzi huwapoka wapiga kura haki ya kumchagua mgombea wanayemtaka.

Ameongeza kuwa vitendo hivyo vya rushwa huwanyima haki baadhi ya wagombea kushiriki na kushindana kwa usawa katika uchaguzi.


Naye Mkuu wa wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai amesema yeye kama Mwakilishi wa Rais katika wilaya hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya TAKUKURU wamejidhatiti kuhakikisha hakuna mtu yeyote atakayechaguliwa kuwa Kiongozi katika wilaya hiyo kwa njia ya rushwa.

" Mtu yeyote mwenye nia ya kugombea katika uchaguzi Mkuu kwa njia ya rushwa, hana nafasi katika Wilaya hii amesisitiza Mhe. Tukai


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila amesema TAKUKURU imewezeshwa vitendea kazi hivyo jukumu walilonalo kwa sasa ni kufanya kazi kwa maslahi ya taifa kabla, baada na hata baada ya Uchaguzi Mkuu


No comments:

Post a Comment