
NA EDWARD WINCHISLAUS
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Carolyne Nombo, amezitaka taasisi za elimu nchini kuiga mfano wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia mfumo wa serikali ya wanafunzi UDOSO Scholarship Fund, unaolenga kufadhili wanafunzi wasiokuwa na uwezo wa kulipa ada.
Prof. Nombo ametoa rai hiyo leo jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfumo huo wa ufadhili wa masomo, ambapo aliwataka wadau wote wa elimu kushiriki kikamilifu katika kuendeleza mfumo huo kwa ubunifu, ushirikiano, na nidhamu katika matumizi ya rasilimali.
"Natoa pongezi kwa serikali ya wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dodoma ya mwaka 2024/2025 kwa wazo la kimkakati, kitaaluma na kizalendo la kuanzisha mfumo wa ufadhili wa masomo—UDOSO Scholarship Fund—kupitia uwekezaji wa hati fungani katika Benki Kuu ya Tanzania," alisema Prof. Nombo.
Aidha, amesisitiza kuwa kila mdau wa elimu, kuanzia wanafunzi, wahadhiri, hadi menejimenti ya vyuo, ana jukumu la kuhakikisha kuwa lengo la mfuko huo linafanikiwa kama lilivyopangwa. Pia, alieleza kuwa mpango huo unaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutoa fursa sawa za elimu kupitia mpango wa Samia Scholarship.

Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa UDOM (UDOSO), Mhe. Jackline Humbaro, akiwasilisha taarifa ya mfuko huo, alisema kuwa baada ya kukamilika kwa mchakato wa uidhinishaji, serikali ya wanafunzi ilinunua hati fungani zenye thamani ya shilingi milioni 100, zenye kipindi cha kuanzia Desemba 2024 hadi Mei 2039.
“Fedha hizo zimetokana na ada za uanachama zinazokusanywa wakati wa usaili kwa wanafunzi wapya. Kupitia uwekezaji huu, mfuko utaweza kuwafadhili takriban wanafunzi 11 kwa mwaka, kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa,” alisema.
Amefafanua kuwa hati fungani ni aina ya uwekezaji wa muda mrefu unaotolewa na serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania, ambapo taasisi au mtu binafsi huwekeza fedha na hulipwa riba kila mwaka hadi muda wa hati hizo kumalizika.
“Lengo kuu ni kuongeza mapato ya serikali ya wanafunzi kwa njia endelevu, salama, na isiyo na hatari kubwa ya hasara, ili kuhakikisha kuwa rasilimali za kifedha zinatumika kwa ufanisi katika kufadhili wanafunzi wenye uhitaji na kugharamia shughuli nyingine za maendeleo,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Mhe. Humbaro amesema UDOSO imejipanga kuimarisha misingi ya kifedha ili kuwanufaisha wanafunzi wote wa sasa na vizazi vijavyo kwa kuweka mkazo kwenye uendelevu na usimamizi thabiti wa rasilimali.

No comments:
Post a Comment