PSPTB YAWATAKA WATAHINIWA KUJIANDAA VIZURI BAADA YA MATOKEO YA MITIHANI YA 30 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, June 20, 2025

PSPTB YAWATAKA WATAHINIWA KUJIANDAA VIZURI BAADA YA MATOKEO YA MITIHANI YA 30



Na Okuly Julius DODOMA


BODI ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imefanikiwa kuendesha mitihani yake ya kitaaluma ya 30 katika vituo saba vilivyopo Tanzania Bara, ambapo jumla ya watahiniwa 1,506 walisajiliwa na 1,421 waliweza kushiriki mitihani hiyo.

Akitoa tathmini ya matokeo hayo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi, alisema jumla ya watahiniwa 680 walifaulu mitihani hiyo, 610 wakitakiwa kurudia baadhi ya masomo, huku 131 wakifeli mitihani yao yote.

Alisema masomo yaliyofanywa vizuri zaidi ni Michakato ya Zabuni na Majadiliano ya Kimkataba, ambapo watahiniwa walionyesha uelewa mkubwa, huku masomo ya hesabu yakiendelea kuwa changamoto kwa wanafunzi wengi.

“Hili linaonesha kuwa kuna umuhimu wa maandalizi ya kina zaidi ili kufikia viwango vinavyokusudiwa na taaluma hii,” alisema Mbanyi.

Bodi imewapongeza watahiniwa waliofanya vizuri na kuwataka wahadhiri kuzingatia miongozo ya ufundishaji inayotolewa na Bodi ili kukuza ubora wa wataalamu wanaozalishwa kwa maendeleo ya Taifa.

Kwa upande mwingine, Bodi imetahadharisha kuhusu ongezeko la udanganyifu kwenye mitihani, ikieleza kuwa baadhi ya watahiniwa walihusika katika vitendo hivyo kutokana na maandalizi hafifu, jambo linalokwenda kinyume na maadili ya taaluma hiyo.

“Ni bora kupata matokeo ya wastani kwa juhudi binafsi kuliko kutumia njia za mkato ambazo zinaweza kukugharimu taaluma yako ya baadaye,” aliongeza Mbanyi.

Aidha, Bodi imewahimiza watahiniwa waliopata changamoto kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya mitihani ya marudio inayotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu, huku wazazi na walezi wakihimizwa kuendelea kuwapa moyo vijana wao katika safari yao ya kitaaluma.

No comments:

Post a Comment