
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa nguzo ya kuimarisha mshikamano na umoja wa kitaifa na kufanikisha maendeleo katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wake, Rais Dkt. Samia ameweza kusimama imara katika kuendeleza miradi ya kimkakati na huduma za jamii, kusimamia demokrasia, kujenga uchumi na kuimarisha diplomasia.
Amesema hayo leo (Alhamisi, Juni 26, 2025) wakati alipotoa hoja ya kukamilisha shughuli za Bunge la 12, Bungeni jijini Dodoma.
“sina shaka nyote mtakubaliana nami kuwa hulka yake na ustahimilivu wake umekuwa faraja kwetu sisi wasaidizi wake, watumishi wote wa umma na Watanzania wote kwa ujumla. Isitoshe, Mheshimiwa Rais wakati wote amekuwa nguzo ya kuimarisha mshikamano na umoja wa kitaifa.”
Amesema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa Mwalimu wa subira, kielelezo cha ujasiri, ustahimilivu na alama ya matumaini kwa kizazi hiki. “Ni kiongozi aliyetoa mfano wa kuwa mwanamke anaweza kuongoza hata kwenye nafasi ya Kitaifa.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kutokana na uongozi dhabiti wa Rais Dkt. Samia, taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa zimetambua mchango na maono yake katika kusimamia shughuli za kimaendeleo nchini na kuitangaza Tanzania nje ya nchi.
Mheshimiwa Majaliwa ametaja tuzo alizopokea kimataifa kuwa ni Global Gates Goalkeepers, Tuzo ya Babacar Ndiaye kwa mwaka 2022, Tuzo ya Uongozi wa Kimageuzi Afrika, Tuzo ya Heshima ya Pyne Africa Awards 2022 na Tuzo ya Muongoza Watalii Bora.
Tuzo nyingine alizopata kitaifa ni Tuzo Maalum ya Heshima ya kutambua mchango wake katika kulitumikia Taifa na kuwaletea wananchi maendeleo iliyotolewa na Bunge, Tuzo Maalum ya kutambua dhamira yake thabiti ya kujenga Taifa linalostahimili Mabadiliko ya Tabianchi.
“Tuzo nyingine alizopata kitaifa ni kutambua mchango wake katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini, tuzo Maalumu ya kutambua mchango, maono na uongozi wake katika kuifanya elimu kama nguzo kuu ya maendeleo ya nchi na tuzo ya Ubinadamu ya kutambua na kuheshimu mchango wake katika masuala mbalimbali yanayogusa jamii ya Watanzania”
Ameongeza kuwa jitihada za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika nyanja mbalimbali zimetoa msukumo kwa wanazuoni katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya Tanzania kumtunuku Shahada ya Juu ya Udaktari wa Heshima.
Ametaja vyuo hivyo kuwa ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru kilichopo New Delhi nchini India, Chuo Kikuu cha Ankara cha nchini Uturuki na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Jamhuri ya Korea.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amewapongeza watendaji wote wa Serikali kwa kutekeleza kwa vitendo maono ya Rais Dkt. Samia. “Leo tunajivunia mafanikio makubwa katika utendaji wa Serikali kwa kila sekta hapa nchini. Mafanikio hayo yanatokana na kujitoa kwao katika kuhakikisha mikakati na maono vinatekelezwa kama ilivyokusudiwa”.





No comments:
Post a Comment