
OR-TAMISEMI
Sanaa za Maonesho ni miongoni mwa michezo inayoshindaniwa katika Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Tanzania kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) yanayofanyika kitaifa mkoani Iringa.
Mashindano haya yanajumuisha vikundi vya ngoma, kwaya, na waimbaji binafsi. Leo Juni 11, 2025, mikoa mbalimbali imeanza kushindana katika fani ya kwaya kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Kleruu, Manispaa ya Iringa.
Leah Kihimbi, Mratibu wa Sanaa za Maonesho kwa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA 2025, amesema sanaa hizi ni jukwaa la kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto katika fani mbalimbali za sanaa.
"Sanaa imebadilika sana siku hizi. Sio tu burudani tena, bali sasa ni ajira rasmi. Tuna mifano hai ya wasanii waliofanikiwa kupitia sanaa, ndani na nje ya nchi. Hapa tunawaandaa wasanii watakaokuwa na taaluma pia," amesema Leah.
Ameongeza kuwa mikoa 26 inashiriki mashindano ya mwaka huu, na anaamini kupitia maonesho haya, vipaji vipya vitazaliwa na kulelewa ili kufikia mafanikio katika miaka ijayo.
Mbali na ngoma za asili na kwaya, Sanaa za Maonesho pia zinajumuisha muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva, unaopata umaarufu mkubwa miongoni mwa vijana.
Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA huandaliwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Kauli mbiu ya mashindano ya mwaka huu ni:
"Viongozi Bora ni Msingi wa Maendeleo katika Taaluma, Sanaa na Michezo – Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu."



No comments:
Post a Comment