
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ya kutatua changamoto za tembo katika Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu huku akimtaka Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina kuwasiliana na Wizara ya Maliasili na Utalii endapo changamoto hiyo itazidi kuwa kubwa.
Mhe. Rais Samia ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Meatu mkoani humo katika viwanja vya Stendi ya mabasi leo Juni 17,2025.
"Kuhusu uvamizi wa tembo, mambo haya yanafanyika hatua kwa hatua kama tumeweza kujenga vituo vitatu vya askari uhifadhi, bila shaka tutaendelea kuchukua hatua zaidi na kama tatizo ni kubwa umuone Waziri wa Maliasili na Utalii" amesisitiza Rais Samia.
Awali, Mhe. Mpina aliiomba Serikali kuweka nguvu kubwa ya fedha kwa ajili ya mikakati ya kupambana na wanyamapori wakali hususan tembo.
Kuhusu Sekta ya Utalii, Rais Samia amesema kuwa kukamilika kwa daraja la Itembe mkoani humo, kutarahisisha watalii kupitia Wilaya ya Meatu kuelekea katika hifadhi za Maswa, Ngorongoro na Serengeti hivyo wananchi wajipange kutumia fursa hiyo.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt.Pindi Chana (Mb), Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii (anayeshughulikia Maliasili ), CP Benedict Wakulyamba, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dkt. Alexander Lobora, Makamishna Uhifadhi wa TANAPA, TAWA , Maafisa Waandamizi kutoka taasisi hizo na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali.






No comments:
Post a Comment