
Na Mwandishi Wetu-Dodoma
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Umoja wa Ulaya (EU) zimejadiliana kushirikiana katika Sekta ya Maliasili na Utalii hususan katika uhifadhi wa mazingira, uchumi wa bluu, ufugaji nyuki na uzuiaji wa uwindaji haramu wa mazao ya misitu na wanyamapori.
Hayo yamejiri katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Mhe, Christine Grau kilichofanyika leo Juni 4,2025 katika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Chana ameomba Umoja wa Ulaya kusaidia uwekezaji wa kiteknolojia na utafiti katika nishati safi ya kupikia, viwanda vya Misitu na kusaidia uanzishwaji wa Maabara ya Sanaa ya Misitu katika Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania – TAFORI.
“ Mlengo wetu ni katika suala la matumizi ya teknolojia katika uhifadhi kwa sababu theluthi ya eneo la nchi ni maliasili hivyo tunapaswa kuhifadhi si kwa faida ya Bara la Afrika tu bali kwa dunia kwa ujumla” amesisitiza Mhe. Chana.
Aidha, Mhe. Chana ameiomba EU kusaidia katika Utekelezaji wa Programu mpya ya Maendeleo ya ufugaji nyuki inayozingatia uboreshaji wa maisha hasa kwa jamii katika utoaji wa ajira hasa kwa vijana na wanawake, kusaidia uhifadhi wa rasilimali za nyuki na maliasili nyinginezo ,kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki na kuuza hasa kwenye soko la kimataifa na kuanzisha awamu ya pili ya mradi wa BEVAC.
Kuhusiana na Sekta ya Misitu Waziri Chana amehimiza na kuwakaribisha wadau mbalimbali kuwekeza katika Biashara ya Kaboni ili kukuza maisha ya jamii na Uchumi wa Taifa huku tukiboresha uhifadhi wa rasilimali zetu za misitu.
Kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya kupikia Mhe. Chana amefafanua kuwa zaidi ya asilimia 90% ya kaya nchini Tanzania zinategemea mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia jambo linalochangia takriban asilimia 54 ya ukataji miti nchini Tanzania hivyo kwa kuwekeza katika nishati safi, kutaepusha ukataji miti hovyo na utunzaji wa ardhi kwa maendeleo ya Taifa.

Naye, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Mhe, Christine Grau amesema kuwa Umoja wa Ulaya uko tayari kutoa ushirikiano wa kutosha katika kuiendeleza Sekta ya Maliasili na Utalii.
“Tumekuwa tukitekeleza programu mbalimbali za uhifadhi katika Sekta ya Maliasili na Utalii ikiwemo shughuli za uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na Pori la Akiba Selous, usimamizi wa jamii za hifadhi za wanyamapori na programu za kuendeleza uchumi wa bluu katika maeneo ya fukwe na Zanzibar.
Amesema pia EU imeanzisha programu ya nishati safi ya kupikia, kusaidia kituo cha taifa cha biashara ya kaboni, kuzuia biashara haramu ya mazao ya misitu na wanyamapori.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ,Alexander Lobora, Mkurugenzi Msaidizi,Idara ya Misitu na Nyuki, Daniel Pancras pamoja na Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.



No comments:
Post a Comment