ukamilishaji wa mradi wa usambazaji umeme katika Vijiji 12,318 umekuwa
kivutio katika Jukwaa la Nishati Afrika linalofanyika nchini Afrika
Kusini.
Kutokana na ufanisi huo unaojumuisha ukamilishaji wa mradi wa umeme wa
Julius Nyerere wa megawati 2, 115 na baadhi ya miradi ya kikanda ya
usafirishaji umeme, imepelekea nchi ya Lesotho kueleza nia yake ya
kuja Tanzania ili kujifunza masuala mbalimbali yatakayoboresha hali ya
umeme nchini humo.
Akizungumza katika Mkutano wa Jukwaa la Nishati Afrika jijini Cape
Town nchini Afrika Kusini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi
Felchesmi Mramba ameeleza kuwa Watanzania wanapaswa kujivunia jinsi
Sekta ya Nishati inavyofanya vizuri na kuwa nchi ya mfano barani
Afrika.
"Watanzania wanaweza wasifahamu sana suala hili lakini Tanzania
inatazamwa sana na mataifa mengine hasa katika eneo la nishati ambalo
tunaendelea kufanya vizuri." Amesema Mhandisi Mramba
Amesema kutokana na sekta ya nishati nchini kufanya vizuri,
Wawakilishi wa Serikali kutoka nchini Lesotho katika Jukwaa hilo la
Nishati Afrika wameeleza nia ya kuhitaji Tanzania kusaidiana nao
katika maeneo yatakayoboresha hali ya umeme nchini humo.
Mramba ameeleza kuwa sekta ya nishati ni sekta muhimu inayoshikilia
uchumi wa nchi kwani kukua kwa uchumi kunategemea uwepo wa nishati ya
kutosha na ya uhakika.
Katika Jukwa hilo la Nishati Afrika, Mramba ameeleza umuhimu wa
kushirikisha sekta binafsi kwenye miradi ya Nishati.
Ametanabaisha kuwa, kutokana na hali ya ukuaji wa uchumi nchini,
Tanzania kwa upande wake inaendelea kuongeza nguvu katika maeneo ya
uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme hivyo ushiriki wa sekta
binafsi ni muhimu.
Katika ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme, amewakaribisha
wawekezaji kuwekeza kwenye eneo hilo akieleza kwamba Serikali pia
imejipanga kuuendelea kuunganisha Tanzania na nchi nyingine ambapo kwa
sasa gridi ya umeme ya Tanzania imeunganishwa na gridi za Kenya,
Rwanda na Burundi na hatua zinazofuata ni kuzifikia Zambia na Uganda.
Katika Jukwa hilo la Nishati Afrika, Watendaji kutoka Tanzania
wamepata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na wawekezaji
mbalimbali walioonesha nia ya kuwekeza Tanzania katika sekta ya
nishati.
No comments:
Post a Comment