MIJI 11 MRADI WA TACTIC KUIMARISHA HUDUMA ZA USAFIRI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 25, 2025

MIJI 11 MRADI WA TACTIC KUIMARISHA HUDUMA ZA USAFIRI





Dodoma


Waziri wa Nchi, Ofisi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kuwa miradi ya TACTIC katika miji 11 inaenda kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji .

Mhe. Mchengerwa ameyasema leo jijini Dodoma wakati wa utiaji saini mikataba 12 ya utekelezaji wa miradi ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) kwa miji ya Morogoro, Songea, Tanga, Korogwe, Babati, Shinyanga, Bukoba, Bariadi, Lindi, Iringa na Njombe.

Amesema miradi hiyo pia inaenda kuimarisha huduma za kiuchumi kwa wananchi hususan upande wa mauzo na manunuzi kwa kuongeza thamani ya biashara nchini ambapo mazingira ufanyaji wa biashara kwenye ngazi za miji na majiji yanaenda kuboreshwa nchini.

“Tunakusudia kuhakikisha kwamba utekelezaji wa miradi hii inatekelezwa kwa wakati, hatuna changamoto ya fedha kwahiyo sitegemei kuona mkandarasi ana legalega”.

“Baadhi ya wakandarasi wakilipwa fedha wanapeleka kwenye miradi mingine, hili sitokubali hata kidogo”, alisisitiza.

Aidha, Waziri Mchengerwa ameonya tabia ya kuchepusha fedha za miradi kunakofanywa na baadhi ya wakandarasi, akiapa kutengua mikataba ya wakandarasi wa namna hiyo katika utekelezaji wa miradi ya TACTIC inayotekelezwa kwenye Miji 45 ya Tanzania bara.

Miradi ya TACTIC iliyosainiwa leo ni ya Miji 11 ya Tanzania Bara, ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa miradi ya TACTIC kwenye miji 45 ambayo imekuwa ikinufaika na ujenzi wa barabara za viwango vya lami, taa za barabarani, mifereji ya maji ya mvua, ujenzi wa vituo vya mabasi na daladala, ujenzi wa masoko ya bidhaa na mazao mbalimbali, bustani za mapumziko pamoja na vivuko vya maji, miradi yote hii ikihusisha takribani Dola za Marekani Milioni 410, bila ya kodi ya Ongezeko la thamani VAT, ikiwa ni Mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.




No comments:

Post a Comment