Na Okuly Julius DODOMA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed O. Mchengerwa amesema jumla ya wanafunzi 214,141 wakiwemo wasichana 97,517 na wavulana 116,624 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi kwa mwaka wa masomo 2025.
Wanafunzi hawa ni kati ya wale waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2024, ikiwa ni pamoja na watahiniwa wa shule za Serikali, zisizo za Serikali na watahiniwa wa kujitegemea.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed O. Mchengerwa (Mb.), wanafunzi 149,818 sawa na asilimia 69.96 ya waliochaguliwa wamepangiwa kujiunga na Kidato cha Tano katika shule 694 za sekondari za Serikali. Kati ya hao, 76,491 ni wasichana na 73,327 ni wavulana.
Wanafunzi 1,728 wakiwemo wasichana 801 na wavulana 927 wamepangwa katika shule nane zenye ufaulu wa juu zaidi; 141,146 (wasichana 72,337 na wavulana 68,809) wamepangiwa shule za bweni; huku 6,944 (wasichana 3,353 na wavulana 3,591) wakipangiwa shule za kutwa.
Aidha, wanafunzi 2,875 (wasichana 1,057 na wavulana 1,818) wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika vyuo vinne vya elimu ya ufundi ambavyo ni: Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Chuo cha Maendeleo ya Maji (WMDI).
Kwa upande mwingine, wanafunzi 2,214 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya afya ngazi ya stashahada, 1,609 kujiunga na vyuo vya ualimu na 57,625 katika vyuo vya kada mbalimbali.
Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa uchaguzi huu umefanyika kwa kuzingatia matokeo ya ufaulu na nafasi zilizopo, hivyo hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko ya shule au chuo kutokana na ukosefu wa nafasi.
Muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano utaanza rasmi tarehe 08 Julai 2025, ambapo wanatakiwa kuripoti kuanzia tarehe 06 Julai hadi mwisho wa kuripoti tarehe 21 Julai 2025. Kwa wanafunzi wa vyuo, watapokea maelekezo ya kujiunga kutoka katika taasisi husika.
No comments:
Post a Comment