WAZIRI WA ULINZI BURUNDI AFANYA ZIARA WIZARA YA ULINZI NA JKT NA KUKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI NA JKT WA TANZANIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 10, 2025

WAZIRI WA ULINZI BURUNDI AFANYA ZIARA WIZARA YA ULINZI NA JKT NA KUKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI NA JKT WA TANZANIA


Waziri wa Ulinzi wa Burundi, Mheshimiwa Injinia Alain Tribert Mutabazi, tarehe 10 Juni 2025, amefanya ziara ya kikazi nchini Tanzania na kutembelea Wizara ya Ulinzi na JKT na kukutana na Uongozi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ulioongozwa na Waziri wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) ofisini kwake jijini Dodoma.

Kikao hicho cha mawaziri wa Ulinzi wa Tanzania na Burundi kilikuwa na lengo la kuzungumzia maeneo mbalimbali ya ushirikiano na kuendeleza ushirikiano wa Diplomasia ya Ulinzi baina ya Tanzania na Burundi,
Waziri Tax alimhakikishia Mhe Waziri Injinia Alain Mutabazi, utayari wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika kuimarisha uhusiano wa muda mrefu baina ya Tanzania na Burundi, katika masuala ya Kijeshi na Usalama kwa ujumla ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za matishio ya kiusalama duniani.

Aidha Mawaziri hao wa Ulinzi wa Tanzania na Burundi walisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Nyanja mbalimbali za Kijeshi baina ya nchi hizo mbili rafiki na majirani.

Baadaye, Waziri wa Ulinzi wa Burundi Mheshimiwa Injinia Alain Mutabazi, alipata fursa ya kutembelea Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, Kikombo na Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma


Viongozi wengine waliohudhuria Kikao hicho cha Mawaziri wa ulinzi wa Tanzania na Burundi ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, viongozi waandamizi toka Wizara ya Ulinzi na JKT na Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment