Zoezi la usambazaji vitabu vya kidato cha tano (Mtaala ulioboreshwa) na cha sita kwa shule za Serikali limeanza rasmi leo Juni 24, 2025 katika ghala la Taasisi ya Elimu Tanzania lililopo External Jijini Dar es Salaam.
Akielezea zoezi hilo Meneja wa uchapaji na usambazaji wa vifaa vya kielimu TET Emmanuel Stanslaus amesema zoezi hilo limeanza katika halmashauri za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambapo walimu wa kuu wa shule wameendelea kujitokeza kuchukua vitabu.
Amesema, zoezi hilo la siku nne limelenga kuhakikisha shule zote 668 za Serikali nchini katika mikoa yote zinapokea vitabu ili kuwasaidia wanafunzi wanaotarajia kuanza masomo yao hivi karibuni.
Aidha, Bw. Stanslaus ametoa rai kwa walimu wakuu wote kufika mapema katika eneo lililoelekezwa ili kuchukua vitabu hivyo kwa haraka kulingana na utaratibu uliopangwa ili wanafunzi waweze kunufaika.
Nae Mwl. Jericko Kisama Rodgers kutoka shule sekondari Mwanalugali ya Kibaha mji Mkoawa Pwani amesema zoezi hilo limekuja wakati sahihi ambapo wanafunzi wa kidato cha tano na sita wanaelekea kufungua shule hivyo litasaidia kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji kupitia Mtaala ulioboreshwa.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Goba ya Jijini Dar es salaam Mwl. Janeth Binagi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha Sekta ya Elimu nchini huku akisisitiza walimu wataendelea kumuunga mkono kwa utendaji wenye viwango.
No comments:
Post a Comment