𝗞𝗪𝗔 𝗔𝗦𝗜𝗟𝗜𝗠𝗜𝗔 99.8 𝗪𝗔𝗝𝗨𝗠𝗕𝗘 𝗪𝗔𝗠𝗘𝗥𝗜𝗗𝗛𝗜𝗔 𝗠𝗔𝗥𝗘𝗞𝗘𝗕𝗜𝗦𝗛𝗢 𝗠𝗔𝗗𝗢𝗚𝗢 𝗬𝗔 𝗞𝗔𝗧𝗜𝗕𝗔 𝗬𝗔 𝗖𝗖𝗠 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, July 26, 2025

𝗞𝗪𝗔 𝗔𝗦𝗜𝗟𝗜𝗠𝗜𝗔 99.8 𝗪𝗔𝗝𝗨𝗠𝗕𝗘 𝗪𝗔𝗠𝗘𝗥𝗜𝗗𝗛𝗜𝗔 𝗠𝗔𝗥𝗘𝗞𝗘𝗕𝗜𝗦𝗛𝗢 𝗠𝗔𝗗𝗢𝗚𝗢 𝗬𝗔 𝗞𝗔𝗧𝗜𝗕𝗔 𝗬𝗔 𝗖𝗖𝗠


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiongozwa na Mwenyekiti wake Dkt. Samia Suluhu Hassan, kimepitisha kwa kishindo marekebisho ya Katiba yake ya mwaka 1977 (toleo la Mei 2025), baada ya kura ya maoni ya ndani ya chama kuonyesha uungwaji mkono wa asilimia 99.8 kutoka kwa wajumbe wa Mkutano Maalum wa CCM uliofanyika Jumamosi kwa njia ya mtandao.

Matokeo ya kura hiyo yalitangazwa rasmi na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Idara ya Oganaizesheni, Issa Haji Ussi Gavu, aliyesema kuwa jumla ya wajumbe 1,915 walishiriki katika upigaji kura, kati ya wajumbe 1,931 waliotarajiwa.

“Idadi ya wajumbe, jumla ya wajumbe wote ambao wanatakiwa kupiga kura hii ni 1931 kama ambavyo tulitangaziwa hapo awali, lakini wajumbe waliohudhuria ni 1915, wajumbe wasiohudhuria ni wajumbe 16, wajumbe waliopiga kura ni wajumbe 1915 lakini kura za hapana ni sifuri, kura zilizoharibika ni tatu, kura za ndiyo ni 1912 hiyo ni sawa na asilimia 99.8.”


Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, awali aliwaeleza wajumbe kuwa marekebisho hayo ni madogo lakini ya kimkakati, na hayana lengo la kubadili mfumo mzima wa uteuzi bali kutoa unyumbufu zaidi kwa Kamati Kuu kuongeza idadi ya wagombea wanaoshiriki kura za maoni.

Marekebisho hayo yaliyoidhinishwa kwa kura hizo ni pamoja na kurekebisha Ibara ya 105(7F) ya Katiba ya CCM kwa kuongezewa kipengele kitakachoiruhusu Kamati Kuu kuongeza idadi ya wagombea wa ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi katika hatua ya kura za maoni, aidha kurekebisha Ibara ya 91(6C) kwa mtiririko huo huo kwa upande wa nafasi za udiwani.

Aidha, Rais Dkt. Samia, amewapongeza wajumbe kwa ushiriki mkubwa na kusema kuwa hatua hiyo inaonesha uimara wa misingi ya demokrasia ndani ya CCM huku akibainisha kuwa mchakato upande wa udiwani utaendelea kama kawaida kwakuwa tayari umesharuka hatua ambayo imefanyiwa urekebu.

No comments:

Post a Comment