DCEA YASHITUKIA MBINU MPYA, MAITI ZATUMIKA KUBEBA DAWA ZA KULEVYA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, July 9, 2025

DCEA YASHITUKIA MBINU MPYA, MAITI ZATUMIKA KUBEBA DAWA ZA KULEVYA




Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imebaini mbinu ambayo baadhi ya wahalifu wa biashara ya dawa za kulevya wameanza kutumia maiti za binadamu kama mifuko ya kubebea dawa hizo haramu.

Aidha, imewakamata watu wawili waliokuwa wamiliki wa kiwanda bubu kilichokuwa kikitengeneza biskuti zilizochanganywa na bangi katika eneo la Sinza jijini Dar es Salaam, ambazo zilikuwa zikisambazwa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Lindi na Mtwara.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema katika operesheni kubwa zilizofanyika kuanzia mwezi Mei hadi Julai mwaka huu, mamlaka yake kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 37,197.142 za dawa za kulevya za aina mbalimbali.

Dawa hizo ni pamoja na kilogramu 11,031.42 za Mitragyna Speciosa (Kratom), bangi kilogramu 24,873.56, mirungi kilogramu 1,274.47, skanka kilogramu 13.42, heroin kilogramu 2.21 na methamphetamine gramu 1.42, pamoja na dawa tiba zenye asili ya kulevya zikiwemo ketamine kilogramu 1.92, vidonge 1,000 vya Rohypnol na lita 6 za hydrochloric acid.

Katika operesheni maalum iliyofanyika bandari kavu ya Temeke jijini Dar es Salaam, amesema mamlaka hiyo ilikamata kilogramu 11,031.42 za Mitragyna Speciosa kutoka Sri Lanka, zilizokuwa zimefichwa kwenye mifuko iliyoandikwa kuwa ni mbolea.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema mmea huo una kemikali hatari zinazoweza kuathiri mfumo wa fahamu na kusababisha uraibu na vifo vya ghafla.

Vilevile, raia wawili wa China, Chein Bai na Qixian Xin, walikamatwa katika eneo la Posta jijini Dar es Salaam wakiwa na methamphetamine gramu 1.42, Rohypnol vidonge 1,000 na ketamine kilogramu 1.92.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema katika kipindi hicho pia, DCEA iliteketeza ekari 1,045.5 za mashamba ya bangi katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Mara, Kagera, Dodoma, Tabora, Morogoro na Arusha, huku ikikamata dawa za mashambani zenye uzito wa kilogramu 26,191.45.

Aidha, mamlaka hiyo iliizuia kuingia nchini kwa kilogramu 26 za heroin zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Msumbiji, na jumla ya watuhumiwa 64 wamekamatwa kutokana na kuhusika na mtandao wa biashara hiyo.

Ameonya kuwa wauzaji wa dawa za kulevya sasa wanatumia pia mbinu za urafiki, kampuni zao na vyombo vidogo vya usafirishaji kama bodaboda, bajaji, teksi na wasambazaji wa vifurushi, ili kuwaingiza Watanzania kwenye biashara hiyo.

Amewataka wananchi kuwa waangalifu wanapotumwa au wanapopokea mizigo kutoka kwa watu wasiowafahamu vyema na kutoa taarifa mapema, huku akisisitiza kwamba serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika na biashara hiyo haramu.

No comments:

Post a Comment