
Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, Akizungumza na Waandishi wa habari Julia 15,2025 jijini Dodoma akielezea kukamilika kwa mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 17, 2025, jijini Dodoma.
Okuly Julius _ DODOMA
Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, ametangaza kukamilika kwa mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 17, 2025, jijini Dodoma.
Akizungumza na Waandishi wa habari Julia 15,2025 jijini Dodoma kuhusu hatua hiyo muhimu , Dkt. Msemwa amesema kuwa mchakato huo umechukua takribani miaka miwili na umehusisha ushirikishwaji mpana wa wananchi, ambapo Watanzania milioni 1.174 walitoa maoni yao kwa njia mbalimbali. Aidha, zaidi ya wananchi 20,000 walihudhuria makongamano ya kitaifa na kutoa maoni yao kuhusu mustakabali wa maendeleo ya Taifa.
"Tulifanya utafiti wa kina kwa nchi zilizopiga hatua na kufikia uchumi wa kati, kwa lengo la kujifunza na kutumia maarifa yao kufanikisha maendeleo tunayoyataka. Malengo ya Tanzania ni kufikia uchumi wa kati kwa njia endelevu," amesema Msemwa.
Ameeleza kuwa Rasimu ya Dira ya 2050 ilirudishwa kwa wananchi kwa ajili ya uhakiki ili kuhakikisha maoni yao yamezingatiwa kikamilifu. Baada ya hatua hiyo, nyaraka hiyo iliwasilishwa katika makundi mbalimbali ya kijamii, kitaaluma na sekta binafsi ili kuhakikisha kuwa hakuna jambo muhimu lililosahaulika.
Msemwa ameongeza kuwa Dira hiyo mpya ya Maendeleo itaanza kutekelezwa rasmi mwezi Julai 2026, mara baada ya kumalizika kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.
Tume ya Taifa ya Mipango, kwa mujibu wa Katibu Mtendaji huyo, ina jukumu la kuratibu mipango ya maendeleo ya Taifa, ikiwemo kuandaa Dira ya Maendeleo na kusimamia utekelezaji wake ili kuhakikisha maendeleo shirikishi, jumuishi na endelevu kwa Watanzania wote.


No comments:
Post a Comment