SEKTA YA MADINI YACHOCHEA MAENDELEO MKOANI TANGA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 15, 2025

SEKTA YA MADINI YACHOCHEA MAENDELEO MKOANI TANGA



Na Okuly Julius _ DODOMA


Sekta ya madini imeendelea kuwa kichocheo kikuu cha maendeleo katika Mkoa wa Tanga, ambapo wananchi wameanza kunufaika moja kwa moja kupitia shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini, huku Serikali ya Awamu ya Sita ikiendelea kuimarisha usimamizi wake katika sekta hiyo.

Akizungumza Julai 15, 2025 jijini Dodoma kwenye mkutano na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, amesema kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya matokeo chanya ya miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

“Ongezeko la wachimbaji wadogo na masoko yaliyosajiliwa limeongeza uwazi na tija katika sekta ya madini, hasa katika wilaya za Handeni, Kilindi na Korogwe,” alisema Dkt. Burian.

Mbali na sekta ya madini, Dkt. Burian amebainisha kuwa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) umetoa matokeo chanya kwa wananchi wa mkoa huo. Alisema kuwa jumla ya walengwa 38,952, sawa na asilimia 57, wameanzisha biashara ndogondogo, huku wengine zaidi ya 48,645 (asilimia 71) wakijiunga na Bima ya Afya (CHF) na kaya 44,234 zikianzisha shughuli za kilimo na ufugaji.

Katika kukuza uchumi, Mkoa wa Tanga unaendelea kutekeleza miradi mikakati ikiwemo ujenzi wa Jengo la Biashara la Dkt. Samia Suluhu Hassan Business Centre, ujenzi wa Soko la Kisasa la Machinga, na Kituo cha Michezo cha TFF eneo la Mnyanjani kwa zaidi ya Shilingi bilioni 4.5.

Dkt. Burian ameeleza kuwa mradi mkubwa wa kimkakati unaotekelezwa kwa kasi ni ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga, ambao ujenzi wake umefikia asilimia 53.

Aidha, fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo imekamilika kwa asilimia 98.7, ambapo wananchi 1,560 kati ya 1,580 wameshalipwa zaidi ya Shilingi bilioni 9.38, na nyumba 43 mbadala zimekamilika kwa asilimia 100.

Mradi huo pia umezalisha ajira zaidi ya 810 katika eneo la Chongoleani na kuibua fursa nyingine za biashara kama mama lishe, usafirishaji na huduma za kifedha.

Kuhusu Bandari ya Tanga, Dkt. Burian asema kuwa maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa gharama ya Shilingi bilioni 429.1 yameongeza ufanisi wa bandari hiyo. Muda wa kuhudumia meli umepungua kutoka siku 5 hadi 2, huku idadi ya meli ikiongezeka kutoka 198 mwaka 2021 hadi 307 mwaka 2025.

Aidha, shehena ya mizigo imeongezeka kutoka tani 888,130 hadi tani 1,191,480 na makasha (TEUs) kutoka 7,036 hadi 7,817, hali iliyoongeza mapato na ajira za muda kwa wakazi wa Tanga.

No comments:

Post a Comment