
MAMLAKA ya Serikali Mtandao (eGA) kupitia Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba imeendelea kuonesha namna Serikali inavyotekeleza mageuzi ya kidigitali kwa lengo la kuboresha utoaji huduma kwa wananchi kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Akizungumza wakati wa Maonesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, Meneja Mawasiliano wa eGA, Subira Kaswaga, amesema kuwa mamlaka hiyo imepewa jukumu kisheria la kusimamia matumizi ya TEHAMA ndani ya Serikali ili kurahisisha utendaji kazi pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Kupitia jukumu hilo la kisheria, tumeweza kutengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA inayosaidia kurahisisha kazi za kila siku serikalini, lakini pia kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa njia ya kidigitali na kwa urahisi zaidi,” amesema Kaswaga.
Akitolea mfano, Kaswaga amesema miongoni mwa mifumo hiyo ni mfumo wa e-Mrejesho, ambao ni jukwaa la kidigitali linalowawezesha wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Serikali kwa njia ya kupeleka maoni, pongezi au malalamiko, huku Serikali nayo ikijibu na kutoa mrejesho wa hatua zilizochukuliwa.
Amesema mfumo huo unapatikana kwa njia tatu, ikiwemo kupitia simu ya mkononi, na unampa uhuru mwananchi kuficha taarifa zake za msingi iwapo hataki kujulikana, huku pia akipatiwa namba ya ufuatiliaji wa taarifa aliyoitoa.
“Kwa mfumo huu, taasisi za umma zinaweza kuona ni malalamiko ya aina gani zinayapokea mara kwa mara, hivyo kumsaidia kiongozi wa taasisi kutambua idara au kitengo kinachosababisha changamoto kwa wananchi, na kuchukua hatua stahiki,” amesema.
Mbali na hilo, mfumo huu pia unasaidia kupima uwajibikaji wa watendaji wa umma kwa kuruhusu ufuatiliaji wa hatua zinazochukuliwa baada ya malalamiko kuwasilishwa. Viongozi wakuu wa Serikali kama Katibu Mkuu Utumishi na Katibu Mkuu Kiongozi wanaweza kuona kwa uwazi taarifa za malalamiko katika taasisi zote za umma.
Kutokana na mafanikio hayo, Subira amesema kuwa mfumo wa e-Mrejesho umeendelea kuipa sifa Tanzania kimataifa, ambapo Julai 7, 2025, mfumo huo ulishinda tuzo ya kimataifa iliyotolewa katika Mkutano wa Dunia wa Jumuiya ya TEHAMA (World Summit on the Information Society – WSIS 2025) katika kipengele cha Serikali Mtandao.
“Ni fahari kubwa kwamba mfumo huu umetengenezwa na Watanzania, na leo unatutambulisha kimataifa. Tunawahamasisha wananchi wautumie mfumo huu ili Serikali iwafikie kwa urahisi na kwa ufanisi,” amesema.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa watumishi wa umma kuhakikisha kuwa maoni na malalamiko yanayowasilishwa kupitia mfumo huo yanashughulikiwa ipasavyo ili kukuza uwajibikaji na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali.


No comments:
Post a Comment